Tanzania yaweka mikakati Mkutano wa COP30

Oct, 07 2025

Tanzania imeendelea na Maandalizi kuelekea Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) utakaofanyika jijini Belem, Brazil Novemba 10 hadi 21, 2025.

Akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa wa Kimkakati uliofanyika Dar es Salaam Oktoba 7,2025 Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amesema mikutano ya awali itasaidia kuweka bayana taswira ya nchi kuelekea COP 30.

"Tuna mambo yetu 14 ambayo tunakwenda kuyasema kuwa msimamo wa Tanzania kuhusiana na masuala mbalimbali na katika kuendelea na mkutano huu tunaangalia na tumeweza kuchambua nafasi ya nchi na tumepata hoja za wadau ili kuiboresha," alisema Msofe.

Ameelaza kuwa katika kikao hiki cha kimkakati wadau wamekumbushwa kuwa masuala ya Nishati, Maji na uharibifu wa Mazingira ni mambo ambayo watakwenda kuyazungumza na lengo ni kwenda kuitangaza Tanzania.

"Dunia imejiwekea utaratibu kukutana na kujadili kwa kina masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na mwaka huu, Tanzania ikiwa mdau wa masuala ya Mazingira duniani itashiriki kupitia uwakilishi wa serikali, taasisi za umma, taasisi binanfsi, mashirika ya Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikalii na wadau wote wanaohusIka na masuala ya Mazingira," aliongeza Prof. Msoffe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) nchini Tanzania Bi. Clara Makenya ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kukutana na kupata uelewa wa pamoja kuelekea COP 30 mkutano unaojumuisha wadau mbalimbali wa Mazingira kutoka maeneo tofauti tofauti.

"Wito wangu kuna mijadala mbalimbali na kila mdau ana jukumu muhimu la kujiandaa kama ni upande wa uchumi wa Buluu, Nishati au eneo lingine ajue eneo lipi anaenda nalo kwa ajili ya kujipanga kimkakati na wadau wa dunia nzima na pia kujua kitu gani anaenda kutoa na kujua mdau yupi anaenda kusapoti agenda anayoiwasilisha na kufahamu kuwa wanaeda kama nchi na kuweza kupata matokeo ambayo yanatarajiwa," alisema Bi. Makenya.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Noel Kaganda amesema kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau wote wa serikali, wadau kutoka sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya kiserikali juu ya maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.Aidha balozi Kaganda ameleza kuwa

"Janga hili la Mabadiliko ya Tabianchi linagusa nchi zote, jamii zote, watu wa hali mbalimbali wenye kipato na wasio na kipato, hivvyo ni jukumu letu kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga ustahimilivu na uendelevu,”

Amesema hilo linaenda na dira ya maendeleo ya nchi ambayo hadi kufukia 2050 inataka kujenga jamii ambayo ni stahimilivi yenye uchumi imara na inayomshirikisha kila mmoja katika jitihada za maendeleo.

Settings