Habari
Tanzania yataka mbinu nafasi ya maendeleo nchi zinazoendelea
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito wa kuwa na mbinu za kimataifa zilizo na uwiano, zinazozingatia usawa na kulinda nafasi ya maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Imesema iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kujenga njia zitakazoleta manufaa kwa watu na mazingira, huku zikiheshimu vipaumbele vya maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Baraka Luvanda wakati akiwasilisha Tamko la Tanzania katika Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa kuhusu Mpito wa Nishati uliofanyika Santa Marta, Colombia Aprili 29, 2026.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na mwelekeo wa haki, jumuishi na unaozingatia maendeleo katika mjadala wa mabadiliko ya mifumo ya matumizi ya nishati duniani, ikitaka njia zitakazozingatia hali halisi za kitaifa na kulinda juhudi za maendeleo ya kiuchumi.
Balozi Luvanda alisisitiza kuwa mjadala kuhusu mabadiliko ya mifumo ya nishati lazima uzingatie usawa, vipaumbele vya maendeleo na tofauti za hali za kitaifa na kueleza kuwa nchi zinazoendelea zinahitaji nafasi ya sera ili kufuata njia zinazolingana na mazingira yao ya kijamii na kiuchumi.
“Malengo ya muda mrefu ya Tanzania yamejikita katika Dira 2050 inayolenga kukuza uchumi wa viwanda, ajira, na kuboresha maisha ya wananchi, mambo yanayohitaji nishati ya uhakika na nafuu,” alisisitiza Balozi Luvanda.
Alisema kupitia Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia na upatikanaji wa nishati kupitia mpango wa ‘Mission 300 Africa’, Tanzania imeimarisha vyanzo mbalimbali vya nishati vikiwemo nishati jadidifu, umeme wa maji, ambazo zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa umeme nchini.
Balozi Luvanda aliongeza kuwa kukamilika kwa Julius Nyerere Hydropower Project kumeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji na kuimarisha uthabiti wa gridi ya taifa na wakati huo nchi inaendelea kuwekeza katika nishati ya jua, upepo na jotoardhi, huku gesi asilia ikiendelea kuwa muhimu katika kusaidia maendeleo ya viwanda na kuhakikisha upatikanaji wa nishati unaotegemewa.
“Kipaumbele kikubwa kwa Tanzania ni upatikanaji wa nishati safi ya kupikia. takribani asilimia 90 ya kaya bado zinategemea kuni na mkaa, hali inayosababisha athari kwa afya, mazingira na ustawi wa jamii, barani Afrika, zaidi ya watu milioni 600 bado hawana umeme, jambo linaloonesha ukubwa wa changamoto ya umaskini wa nishati,” alisema.
Pia, Balozi Luvanda alibainisha kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini ya kimakakati yanayohitajika katika teknolojia za nishati safi, ikiwa ni pamoja na yale yanayotumika katika nishati jadidifu na uhifadhi wa umeme.
Alieleza kuwa Serikali inaendeleza sera za kuongeza thamani (beneficiation) na uchakataji wa madini hayo ili kuhakikisha yanachangia kikamilifu katika maendeleo ya viwanda na ukuaji shirikishi wa uchumi.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zilizoalikwa kushiriki katika mkutano huo wa ngazi ya juu, jambo linaloonesha nafasi yake muhimu katika mijadala ya kimataifa kuhusu nishati.



