Habari
Tanzania na UNEP kuimarisha ushirikiano uhifadhi wa mazingira, ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amefanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Bw. Daniel Pouakouyou, anayeshughulikia miradi ya Miradi ya Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environment Facility (GEF)) katika maeneo ya hifadhi ya bioanuai na uongoaji wa ardhi. Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Nairobi, Kenya, pembezoni mwa mikutano ya SBSTTA-28 na SBI-7 chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Hifadhi ya Bioanuai.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Muyungi ameishukuru UNEP kwa ushirikiano wa muda mrefu na Serikali ya Tanzania, hususan katika utoaji wa msaada wa kitaalam na kifedha katika utekelezaji wa miradi ya mazingira, bioanuai, urejeshwaji wa mifumo ikolojia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia Mifuko ya GEF na Green Climate Fund (GCF).
Dkt. Muyungi ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha jitihada za uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inatambua usimamizi endelevu wa maliasili, uhifadhi wa mazingira, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na uchumi wa kijani kuwa msingi muhimu wa maendeleo jumuishi na endelevu.
Kupitia mazungumzo hayo UNEP na Ofisi ya Makamu wa Rais zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kuandaa miradi itakayopata fedha kutoka Mzunguko wa 9 wa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF-9) ikiwemo Miradi wa kipaumbele chini ya Programu ya Mageuzi ya Hifadhi ya Mazingira kuelekea Dira 20250 itakayotekelezwa kati ya 2026–2030.
Maeneo mengine ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni pamoja na kutambua na kuweka ramani ya fursa za miradi ya biashara ya kaboni nchini; kuendeleza mipango ya matumizi ya maeneo ya bahari (Marine Spatial Plans) na mfumo wa usimamizi jumuishi wa maeneo ya pwani; kuandaa kanzidata ya kitaifa ya taka za plastiki katika mazingira ya nchi kavu na baharini; pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Akihitimisha Dkt Muyungi alisema “Tanzania inathamini ushirikiano wake na UNEP na tunaamini mazungumzo haya yatafungua fursa zaidi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira, bioanuai na ustahimilivu wa nchi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kuelekea kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,”



