Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Makamu wa Rais

Serikali yaweka mikakati kuimarisha usimamizi wa taka

Mar, 30 2026

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taka kwa kuandaa Mkakati wa Taifa wa usimamizi wa Taka (2025 - 2030) ambao unalenga kupunguza uzalishaji wa taka kwa kutumia dhana ya uchumi rejeshi.

Katika kuhakikisha mnyororo wa usimamizi wa taka unaimarika, Serikali inahamasisha wadau hususan sekta binafsi kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa za kuchakata taka, uwekezaji katika viwanda vya urejelezaji na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa taka ili kufikia malengo ya kupunguza au kuondoa taka katika Mazingira kwa kuigeuza kuwa malighafi ya uzalishaji wa bidhaa anuwai zinazofaa kwa matumizi mbalimbali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri, Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, Machi 30, 2026.

Amesema Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri huadhimishwa kila mwaka Machi 30 kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kupunguza matumizi ya bidhaa zinazopelekea kuzalisha taka, kutumia tena bidhaa kabla ya kugeuzwa taka na kuchakata taka kwa kurejeleza ili kuepuka uchafuzi wa mazingira.

“Kauli mbiu ya kimataifa kwa mwaka huu inatoa hamasa ya "KUWEZESHA TAKA SIFURI KWENYE SEKTA YA CHAKULA" ikiwa na lengo la kuhimiza matumizi endelevu ya vyakula na kupunguza taka zitokanazo na sekta hii. Kwa upande wa Tanzania, kauli mbiu ya Kitaifa inahimiza kutambua "TAKA NI FURSA" ikisisitiza kuwa taka si uchafu bali ni malighafi yenye thamani, endapo itasimamiwa na kuchakatwa vyema.”

“Uzalishaji wa taka umekuwa changamoto kubwa kwa nchi za Ugaibuni na Africa, hususani katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Arusha na takwimu zinaonesha takribani kiasi cha tani zaidi ya millioni 7 za taka ngumu huzalishwa nchini kwa mwaka ambapo wastani wa asilimia 45 hadi 50 tu hukusanywa na kutupwa dampo.

Aidha, amesema asilimia 50 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mito na mifereji ya maji taka na mitaro ya maji ya mvua. Hata hivyo, matokeo ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonesha kuwa, asilimia 40 ya kaya zinachoma taka ngumu na asilimia 22 ya kaya zinatumia njia ya ukusanyaji sahihi wa mara kwa mara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware amesema ni wakati sasa wa kubadili mtazamo kuwa taka si uchafu tu bali ni rasilimali yenye thamani.

Amesema mabaki ya chakula yanaweza kuzalisha mbolea na nishati, plastiki inaweza kurejelezwa na kuwa bidhaa mpya, na chuma chakavu kinaweza kurejelezwa na kuzalisha bidhaa nyingine.

“Ninatoa wito kwa kila mmoja wetu kuanzia maeneo ya makazi, biashara na viwandani kuchukua hatua madhubuti za kupunguza uzalishaji wa taka, kuchambua taka katika vyanzo vyake na kuimarisha utamaduni wa kuchakata taka.”

Habari

Settings