Prof. Msoffe: Matokeo ya tafiti yalete suluhisho uharibifu wa udongo

Dec, 03 2025

Watafiti nchini wametakiwa kuhakikisha matokeo ya tafiti zinazofanywa zinaleta majawabu ya kisayansi kwa wananchi hususan katika kupunguza uharibifu wa ardhi au udongo kwa kurejesha ardhi iliyoharibika.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe alipomwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja katika Maadhimisho ya Siku ya Udongo Duniani Kitaifa katika Viwanja vya Nane Nane jijini Dodoma leo Desemba 03, 2025.

Prof. Msoffe amesema kuwa ili kuleta tija katika sekta ya kilimo nchini watafiti hao wanapaswa kuhamasisha njia bora za kilimo zinazolinda udongo na mazingira kwa ujumla.


Akiwasilisha mada katika mjadala wakati wa maadhimisho hayo alisema Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ina dhamana ya Uratibu na Usimamizi wa Mazingira nchini itaendelea kuandaa Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati na Programu madhubuti zinazolenga kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.

Naibu Katibu Mkuu Prof. Msoffe alisisitiza kuwa afya ya udongo ni muhimu katika utunzaji wa mazingira hivyo hauwezi kuzungumzia uhifadhi wa mazingira bila kuzungumzia afya ya udongo.

Hivyo, alipongeza jitihada zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika kuhakikisha kuwa masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira yanajumuishwa katika mjadala huo muhimu.


Maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 yameandaliwa na TARI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakichagizwa na Kaulimbiu isemayo ‘Afya Bora ya Udongo kwa Majiji Maridhawa’.

Vilevile, katika kuhakikisha Maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza masuala mbalimbali kuhusu Afya ya Udongo, yameambatana na Mjadala (Panel discussion) ambapo Prof. Msoffe alikuwa miongoni mwa watoa mada akiangazia masuala ya Utunzaji wa Mazingira na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Afya ya Udongo.


Settings