Habari
Naibu Waziri Kwagilwa afunga kiwanda kwa ukiukwaji sheria ya mazingira
Kiwanda cha kuzalisha nondo cha Hangjin Steel Tanzania Limited kilichopo Kisenvule, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, kimefungwa kwa muda baada ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, kubaini ukiukwaji wa sheria za mazingira pamoja na kukutwa kwa risasi ambazo hazijatumika ndani ya eneo la kiwanda hicho.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa kushtukiza, Mhe. Kwagilwa amesema pamoja na kiwanda hicho kutokuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment - EIA) kutoka NEMC, pia kilibainika kutiririsha oil chafu, maji machafu na taka hatarishi nje ya eneo la uzalishaji, hali inayohatarisha afya za wananchi na mazingira yanayokizunguka.
Katika ukaguzi huo, viongozi hao walikuta risasi ndani ya kiwanda hicho zikiwa zimehifadhiwa kwenye ndoo jambo lililoibua wasiwasi wa kiusalama kutokana na hali hiyo Mhe. Kwagilwa amemtaka Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kufuatilia kwa kina chanzo, idadi na matumizi ya risasi hizo kwa mujibu wa taratibu za vyombo vya dola.
“Pamoja na mambo yote hayo niliyoyaelezea, hizi ni risasi ambazo hazijatumika na hapa tumezikuta kwa uchache. Hatujui ni risasi kiasi gani zipo hapa wala zinatumika kwa shughuli gani. Bahati nzuri Kamanda OCD upo hapa, naelekeza mlifuatilie suala hili kwa taratibu zenu za kiusalama,” alisema Mhe. Kwagilwa.
Aidha, Naibu Waziri ameeleza kusikitishwa na hali ilivyofikia huku akiihoji NEMC kwa nini ukiukwaji huo uliendelea kwa muda mrefu, ingawa maafisa wa Baraza hilo walieleza kuwa mara kadhaa walizuiwa kuingia kiwandani na kukosa ushirikiano kutoka kwa uongozi wa kampuni hiyo hata walipowaita ofisini.
Kutokana na ukiukwaji huo, Mhe. Kwagilwa ameamuru shughuli zote za uzalishaji katika kiwanda hicho kusimamishwa mara moja hadi kitakapotekeleza matakwa yote ya kisheria ya NEMC, akisisitiza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitavumilia wawekezaji wanaoharibu mazingira na kuhatarisha usalama wa wananchi kwa kuwa ulinzi wa mazingira ni wajibu wa kulinda vizazi vya sasa na vijavyo.



