Habari
Mpango kazi Uchumi wa Buluu kunufaisha wananchi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Mpango kazi wa Utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu unaweka misingi imara ya kuinufaisha Tanzania kutokana na sekta hiyo.
Amesema hayo wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Mawaziri wa sekta zenye mnasaba wa masuala ya uchumi wa buluu kilichofanyika jijini Dodoma Aprili 16, 2026.
Mhandisi Masauni alisema Tanzania ina fursa nyingi kupitia sekta hiyo ambazo zinaweza kuwanufaisha wananchi kwa kuwawaezesha kujipatia ajira kwa kufanya shughuli za kuingiza kipato na hivyo kuchangia uchumi wa nchi.
Aliwaomba mawaziri wote kuungana kwa pamoja na kushirikiana kupitia wataalamu waliopo katika wizara zao zenye mnasaba wa uchumi wa buluu kushiriki katika kuufanyia kazi mpango kazi huo ili uwe endelevu.
“Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais ni waratibu na wenye sekta ni ninyi mawaziri kupitia wizara zenu hivyo tunaomba ushirikiano wenu ili kupata wataalamu kutoka sekta mbalimbali kuufanya mpango huu uweze kuwa na tija madhubuti,” alisisitiza Masauni.
Wakichangia wakati wa kikao hicho mara baada ya mawasilisho kuhusu utekelezaji na Mpango kazi Jumuishi wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu, Mawaziri walishauri itolewe zaidi elimu kuhusu sekta hiyo na fursa zilizomo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafidh Ameir walishauri mpango huo ushirikishe wadau mbalimbali.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Dkt. Festo Dugange alisema ni muhimu kuhusisha ngazi za chini katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uchumi wa buluu.
Alisema katika ngazi za Serikali za Mitaa kuna wadau wakiwemo maafisa uvuvi na maliasili ambao wanaweza kushirikishwa na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia maafisa viungo.
Nae Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Mathew alisisitiza uimarishaji wa uratibu wa sekta ili kuhakikisha matumzi ya rasilimali za maji unafanyika bila kusababisha migongano ya kimatumizi.
Awali akitoa neno la utangulizi Katibu Mkuu Ofisi ya Majkamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi alisema kwa kuandaa mpango huo kutasaidia kuwa na uelekeao wa kutumia uchumi wa buluu kwa uhakika na kwa manufaa kama ambavyo Dira ya Taifa ya Maedneleo 2050 inavyoeleza.
Dkt. Muyungi alibainisha kuwa baada ya kuunda Kitengo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuna mambo mengi ambayo yamefanyika na yatakayofanyika.
Alisema kupitia kikao cha makatibu wakuu kiliangalia mambo matatu yamezingatiwa ambayo ni utekelezaji wa shuguli wa taasisi na idara kwa miezi sita, mambo ya msingi kwa mwaka ujao kwa maana ya uratibu na shughuli zake pamoja.
Katika kikao hicho mawaziri walipokea na kupitisha taarifa ya utekelezaji wa
Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu kwa kipindi cha Julai hadi Desemba
2025, Mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu
kwa mwaka 2026/27 na Mpango kazi wa uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Maji (2025–2030).



