Habari
Matumizi ya nishati safi ya kupikia yafikia asilimia 92 kambi za jeshi
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imechukua hatua za utunzaji wa mazingira kwa taasisi zake kutumia nishati safi ya kupikia na kupanda miti 209,794 katika kambi mbalimbali za jeshi nchini katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kambi zake zinazolisha zaidi ya watu 100 yamefikia asilimia 92 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, JKT imefikia asilimia 100.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2026 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Alifafanua kuwa taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara hiyo zimeendelea kufanya maboresho katika matumizi ya nishati safi na kusema Shirika la Mzinga limefikia asilimia 98 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia huku Tanzania Automotive Technology Center nalo likifikia asilimia 98.
Dkt. Nyasaho alisema Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutekeleza mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kambi zote za JKT nchini.
Alitaja shughuli hizo kuwa ni utengenezaji wa mashine za kuzalisha mkaa mbadala, ujenzi wa miundombinu ya mitambo ya gesivunde (biogas) katika baadhi ya vikosi vya JKT pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu utengenezaji wa mkaa banifu katika kambi mbalimbali.
Aidha, Waziri huyo alibainisha kuwa Wizara imeendelea kuchukua hatua za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya jeshi yenye misitu ya asili kwa kuyakinga dhidi ya uvamizi wa shughuli za kibinadamu pamoja na kuendelea kupanda miti mipya.
Itakumbukwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitangaza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuanzia Januari 2024 ambapo taasisi hizo zilianza kutekeleza maelekezo hayo na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanachangia ukataji wa miti yanayosababisha uharibifu wa mazingira.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kunusuru miti inayokatwa ambapo inakadiriwa kila mwaka takriban hekta laki nne za misitu zinapotea kutokana na kukatwa kwa ajili ya kuni na mkaa.



