Habari
Makamu wa Rais ataka kufufuliwa kilimo cha maua Arusha, ahimiza ushiriki wa vijana katika kilimo
Ndejembi amesema hayo leo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa na Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, katika viwanja vya TGT, Halmashauri ya Arumeru - Arusha.
Amesema mauzo hayo yameongezeka kutoka dola milioni 290.7 mwaka 2020, huku tasnia hiyo ikikua kwa wastani wa asilimia tisa hadi 12 kwa mwaka.
Amesema taratibu za kufungua masoko mapya zitaendelezwa mwaka wa fedha 2026/2027, sambamba na kuwajengea uwezo wakulima kukidhi viwango vya kimataifa. Akitembelea mabanda kabla ya ufunguzi, ameielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kubaini bidhaa zinazohitajika katika masoko hayo na viwango vyake vya ubora ili kuwaongoza wazalishaji.
Amesema uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka tani milioni 8.44 mwaka 2022/2023 hadi tani milioni 9.78 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 15.9. Kwa upande wa parachichi, uzalishaji umefikia tani 203,473 mwaka 2025/2026, kutoka tani 149,340 mwaka 2020/2021, huku kiasi kinachouzwa nje kikifikia tani 52,593.72 zenye thamani ya Sh bilioni 255.4.
Kutokana na fursa hizo, Ndejembi ameielekeza Wizara ya Kilimo kuimarisha uzalishaji wa miche bora, uhifadhi wa mazao na utoaji wa mafunzo ili kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo cha parachichi.
Aidha, ameitaka wizara hiyo kufufua kilimo cha maua kwa kutumia mashamba yaliyopo Arusha yenye miundombinu ya uzalishaji. Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya fedha za kigeni, akikumbusha kuwa maua yaliyozalishwa Arusha hapo awali yalikuwa na soko kubwa duniani.
Amepongeza mchango wa Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA) katika kuwawezesha wakulima na wajasiriamali, akitolea mfano kampuni ya Onocado Farm. Kampuni hiyo inaongozwa na kijana aliyesaidiwa na TAHA kuingia katika kilimo cha parachichi na sasa anasafirisha nje zaidi ya tani 430 kwa mwaka.
Ndejembi amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika uzalishaji, pembejeo, uchakataji, usafirishaji na uhifadhi wa mazao kwa ubaridi. Amesisitiza kuwa kupunguza upotevu wa mazao na kuunganisha uzalishaji na masoko kutasaidia bidhaa kuwafikia wanunuzi kwa wakati, zikiwa na ubora unaotakiwa na kwa gharama zinazowawezesha wakulima na wafanyabiashara kupata faida.
Akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema wizara imejizatiti kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani ili kuongeza pato la Taifa na mapato ya fedha za kigeni, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Chongolo amesema wizara, kwa kushirikiana na sekta binafsi, itaendelea kuwawezesha vijana na wanawake kujiajiri kupitia mafunzo na mikopo, sambamba na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na huduma za ugani ili kuongeza tija katika mazao ya chakula na biashara.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TAHA, Johannes Cornelius Bogers, amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika matunda, viungo, maua na mbogamboga. Amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa mitaji na ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi ili kuvutia uwekezaji zaidi katika uzalishaji, usafirishaji na masoko.
Maonesho ya HortiLogistica Africa 2026 wamehudhuriwa na nchi 45 na yanafanyika Novemba 8 hadi 10 mkoani Arusha, yakiwa na kaulimbiu ya “Kuunganisha Masoko, Kukuza Ustawi”. Yanawakutanisha wakulima, wanunuzi, wasafirishaji, wasindikaji, wawekezaji na watoa huduma za teknolojia kutoka Afrika na masoko ya kimataifa.



