Habari
Kwagilwa awasihi wadau kuwekeza ubunifu kulinda mazingira
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ametoa wito kwa wadau kuendelea kuwekeza katika ubunifu wa teknolojia ili kuimarisha juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa wito huo wakati akifungua Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma Juni mosi, 2026.
Mhe. Kwagilwa alisema pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, Watanzania wameonesha namna wanavyounga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto hizo kwa kufanya ubunifu wa teknolojia, matumizi ya sayansi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi wa mazingira kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazosaidia kuongeza ufanisi katika uhifadhi wa rasilimali za asili na kukabiliana na changamoto za tabianchi.
“Hatupaswi kuendelea kulalamikia athari za mabadiliko ya tabianchi na badala yake ni lazima tuendelee kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na athari hizo zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mhe. Kwagilwa.
Aidha, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa nguzo ya tatu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka msisitizo katika uhifadhi wa mazingira na kuongeza uwezo wa Taifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika, aliipongeza Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia muswada wa Sheria mpya ya Mazingira Namba 191 kuwasilishwa bungeni Septembe mwaka huu ambayo itawezesha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa Mamlaka kamili, hatua itakayoongeza chachu katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Naibu Waziri Kwagilwa alisisitiza kuwa sheria hiyo iyaguse mambo yote ya msingi ambayo yatasaidia kama nchi au Serikali kuweka udhibiti madhubuti na uhifadhi endelevu wa mazingira.
Hivyo, Mhe. Kwagilwa aliwasihi wananchi, taasisi na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira na kusisitiza kulinda na kuhifadhi mazingira.
Awali akizungumza, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda alisema maonesho hayo yatahusisha wadau mbalimbali wa mazingira watakaoonesha teknolojia, ubunifu na elimu.
Alieleza kuwa pia, maonesho ni njia mojawapo ya kuchangia kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutumia rasilimali za asili kwa njia endelevu.
Balozi Luvanda alisema kuwa wananchi watajifunza kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kukabiliana nazo.
Katika ufunguzi wa Maonesho ya Maaadhimisho ya Siku Mazingira Duniani, ni takriban mabanda 20 kati ya 80 yalitembelewa na mgeni rasmi na washiriki wake kutoa maelezo kuhusu namna wanavyoshiriki katika kulinda na kuhifadhi ya mazingira.
Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na taasisi zilizo chini yake zikiwemo NEMC na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) inashiriki na kutoa elimu kuhusu sekta za Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu ambazo inazisimamia.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu 'Dira 2050; Tuwajibike kukijanisha Tanzania' na kilele kinatarajiwa kufanyika Juni 05, 2026 ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.



