Habari
Kamati ya Bunge yataka mradi wa biashara ya kaboni itanue wigo Iringa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imependekeza kutekelezwa kwa mradi wa biashara ya kaboni katika vijiji vinavyozunguka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ili kujenga hamasa ya utunzaji mazingira.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) katika Halmashauri ya Iringa.
Mhe. Kiswaga amesema kwa vile eneo hilo limezungukwa na msitu hivyo ipo haja ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuangalia uwezekano wa kuwepo na mradi wa biashara ya kaboni.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiwa wameambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange na watendaji wa ofisi hiyo walitembelea Mfereji wa Skimu ya umwagilia yenye urefu wa mita 3,500 una thamani shilingi milioni 86 na ujenzi wa jengo la kiwanda kidogo cha kuchakata mahindi wenye thamani ya shilingi milioni 116.6.
Akizungumza wakati wa kutembelea miradi hiyo, Mhe. Kiswaga alisema kamati imeridhishwa na utekelezaji wake na kuwa inaleta manufaa kwa wananchi kwa kuwaingizia kipato kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kwa upande wake, Dkt. Dugange alisema Ofisi hiyo inatekeleza miradi ya mazingira ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli mbadala zizikuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Alisema pamoja na mradi huo wananchi wanapaswa kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha mafuriko, ukame na maradhi.
Nae Mratibu wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) Dkt. Damas Mapunda alisema matokeo ya mradi huo ni mazuri hiuvyo wanatarajiwa kuja na awamu ya pili ya utekelezaji
Mradi huo pia unatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya za Wanging’ombe, Mbarali na Mbeya katika bonde la Ruaha Mkuu na halmashauri za Sumbawanga, Mpimbwe na Tanganyika katika Bonde la Ziwa Rukwa.
Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira iliwashirikisha pia Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Balozi Baraka Luvanda na watendaji kutoka Ofisi hiyo.



