Habari
Dkt. Muyungi: Ofisi ya Makamu wa Rais kuwawezesha vijana kunufaika na miradi ya mazingira
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imepanga kushirikiana na Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana hatua inayolenga kuwawezesha vijana kunufaisha na fursa za miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano (Januari 28, 2026) Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Richard Muyungi wakati wa kikao baina yake na msanii wa muziki wa kikazi kipya (Bongo Flavour) na mtangazaji wa Kituo cha Redio cha Clouds FM, Bi. Frida Amani.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanzisha Wizara maalum ya Vijana inayolenga kubainisha fursa zitakazowanufaisha vijana ikiwemo programu za miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
“Hivi karibuni nimekutana na taasisi ya vijana ya Green Samia Foundation ambapo nimewasihi kuchangamkia fursa zinazohusiana na uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwani ina fursa zinazoweza kuwaletea maendeleo yao” amesema Dkt. Muyungi.
Dkt. Muyungi Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kushirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii yanayoshiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo vijana hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za makundi hayo.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Muyungi apongeza juhudi na jitihada mbalimbali zinazofanywa na msanii huyo pia ni Balozi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa kuendelea kujenga hamasa ya uhifadhi wa mazingira kupitia tasnia ya muziki na utangazaji.
Aidha Dkt. Muyungi amemwomba Balozi huyo kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais katika shughuli za matukio mbalimbali ya kitaifa na kimatifa ikiwemo maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani (WED) na Mikutano ya Nchi Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP).
Aidha ametoa ushauri kwa msanii huyo kutangaza pia maeneo ya uhifadhi yaliyopo nchini na kuitaja hifadhi ya taifa ya Saadani ambayo ina utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii, wanyamapori na fukwe za kupendeza
“Nashauri pia tuitangaze hifadhi ya taifa ya Saadani ambayo mbali na vivutio vya utalii na wanyamapori na pia kuna tukio la kipekee ambalo unawakuta wanyama wakipunga upepo katika fukwe zilizopo ndani ya hifadhi hii,” amesema Dkt. Muyungi.
Kwa upande wake, Balozi huyo wa UNEP, Bi. Frida Amani ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutambua mchango na juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuhamasisha masuala ya urejeshaji wa mifumo ikolojia.
Amesema hadi kufikia sasa taasisi yake ya The Amani Foundation imetekeleza programu mbalimbali za urejeshaji wa mifumo ikolojia ikiwemo kushiriki katika zoezi la upandaji wa miti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Naye Meneja wa Msanii huyo, Frank Mkuvalwa amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika urejeshaji wa mifumo ikolojia taasisi hiyo imekuwa ikiandaa matamasha na mabonanza mbalimbal yanayolenga kuhamasisaha jamii umuhimu wa kutunza mazingira.
Amesema kupitia taasisi ya The Amani Foundation, imeweza kushirikiana na taasisi na watu mashuhuri ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusu umuhimu wa masuala ya urejeshaji wa mifumo ikolojia nchini.
“Tumepanga kuwa na matukio makubwA kwa mwaka huu ambayo yanahamasisha umuhimu wa uhifadhi wa mifumo ikolojia ambapo msanii wetu Bi. Frida Amani amepanga kutunga wimbo mmoja ndani ya msitu huo ya msitu wa Pugu” amesema Mkuvalwa.



