Habari
Dkt. Muyungi aiasa NEMC kusimamia utekelezaji wa sheria
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo amekutana na Menejimenti ya Baraza kwa lengo la kujitambulisha na kujionea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.
Katika kikao kilichohusisha pia Mameneja wa Kanda 13 nchi nzima kiliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Baraza, ikiwemo mafanikio yaliyofikiwa, changamoto za mazingira zinazojitokeza pamoja na hali ya mazingira kwa ujumla.
Aidha, ziliainishwa pia fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya mazingira hususani eneo la urejelezaji wa taka zinazoweza kuvutia uwekezaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi endelevu wa mazingira.
Dkt. Richard Muyungi alipozungumza ameishukuru NEMC kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhifadhi na kusimamia mazingira ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sheria
Amesisitiza umuhimu wa Baraza kuzingatia mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mahitaji ya sasa ya jamii ili kuendana na ulimwengu wa kidigitali katika kufikisha elimu ya Mazingira kwa jamii.
Aidha, Dkt. Muyungi ameitaka NEMC kuanzisha kitengo cha Ubunifu kitakachokuwa na jukumu la kubuni na kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mazingira, ikiwemo kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia bunifu na endelevu.
Vilevile amesisitiza kuzingatiwa kwa weledi katika uchakataji na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na misingi ya uhifadhi wa mazingira.



