Habari
Balozi Luvanda aipa kongole NEMC
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Baraka Luvanda amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa mikakati iliyojiwekea kutekeleza malengo ya nguzo ya tatu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Mhe. Luvanda amesema hayo leo Alhamisi Machi 05, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kujitambulisha na kuzungumza na Menejimenti ya Baraza hilo sambamba na kufahamu majukumu yanayotekelezwa na Ofisi hiyo.
Mhe. Luvanda amesema NEMC imebeba maono na matarajio makubwa ya nchi katika kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya taifa 2050 hususani utelekelezaji wa nguzo ya tatu inayoakisi masuala ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa taarifa nilizoona nimeridhishwa na utayari wenu katika utekelezaji wa dira 2050…..Hatuna budi kutambua kuwa tumebeba matumaini ya Viongozi wakuu wa kitaifa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050 katika upande wa mazingira” amesema Mhe Balozi Luvanda.
Aidha Mhe. Balozi Luvanda amesema suala la elimu kwa umma halina budi kupewa kipaumbele na msukumo wa pekee ili kuhakikisha inapatiwa uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa ajili ya mustabali endelevu wa taifa.
Balozi Luvanda pia ameishauri Menejmenti ya NEMC kuweka msukumo wa kujitangaza kwa jamii na wadau mbalimbali kwa kuwa misingi ya utekelezaji wa jukumu hilo limeanishwa katika sheria na kanuni zinazosimamia majukumu ya taasisi hiyo.
Mhe. Balozi Luvanda amesema NEMC ni taasisi muhimu yenye mchango mkubwa katika kuharakisha kasi ya ukuaji wa sekta za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini na hivyo ana imani na watendaji wa ofisi hiyo katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware amemshukuru Mhe. Balozi Luvanda kwa ziara hiyo ya kikazi katika ofisi za baraza hilo na kuwa ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano ili kuwezesha na kufanikisha dhamira na maono ya Serikali.
“Sisi kama Watumishi wa NEMC tunakukaribisha Mhe. Balozi Luvanda tutambua majukumu uliyonayo yanaakisi shughuli zinazotelekezwa na NEMC, hivyo tupo tayari kupokea maelekezo na kufanyia kazi” amesema Dkt. Sware.
Mhe. Balozi Baraka Luvanda aliteuliwa hivi karibuni na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais akichukua nafasi ya Prof. Peter Msoffe aliyehamishiwa Wizara ya Kilimo.



