Dkt. Kijaji: Halmashauri kujenga vituo cha kuchakata taka ngumu

Aug, 15 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatarajiwa kujenga vituo vya kuchakata taka ngumu kwa lengo la kupunguza kiasi cha taka zinazokwenda dampo.

Amesema hatua hiyo ni kutokana na Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Taka Ngumu za Mwaka 2024 zinazoelekeza wazalishaji wa bidhaa wawajibike na taka wanazozalisha kupitia dhana ya Mazingira na maendeleo endelevu, kuanza kufanyiwa mapitio na Serikali.

Dkt. Kijaji amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa zoezi la urejelezaji wa taka ngumu katika Jiji la Dar Es Salaam kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Agosti 15, 20204.

Amesema uzalishaji wa taka ngumu unakadiriwa kuwa takribani tani milioni 7 kwa mwaka na kiasi kikubwa kinazalishwa katika Mamlaka za Majiji, Manispaa na Halmashauri za Miji Midogo ikilinganishwa na Halmashauri za Wilaya ambazo nyingi ziko vijijini.

Aidha, urejelezaji wa taka ngumu ni moja ya mbinu ya upunguzaji wa taka katika madampo ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 5 hadi 10 ya taka ngumu

zinazozalishwa nchini zinarejelezwa zikiwemo za plastiki, karatasi, chuma

chakavu, makopo ya aluminiamu na chupa za kioo.

“Shughuli hizi za urejelezaji ni mojawapo ya mikakati ya kuboresha usimamizi wa taka ngumu na kupunguza kiasi cha taka ngumu zinazopelekwa dampo. Hatua hii ni muhimu kwa kuzingatia kuwa taka ngumu zinaweza kuwa malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine pamoja na kutoa fursa za ajira na hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kulinda afya ya jamii pamoja na kuboresha hifadhi ya mazingira,” amesema.

Dkt. Kijaji amesema uwepo wa kiwango kidogo cha taka zinazorejelezwa unatokana na mwitikio mdogo wa utenganishaji wa taka katika ngazi ya kaya na maeneo ya biashara, masoko, viwanda na taasisi katika maeneo mengi ya jiji na Manispaa.

Hivyo, hali hiyo inawekewa msukumo kwa kukuza uelewa wa jamii na wakazi wa jiji kuhusu umuhimu wa utenganishaji wa taka ili kuwezesha zinazoweza kurejelezwa kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kupitia kwa Mwenyekiti Mhe. Jackson Kiswaga, Mhe. Dkt. Bashiru Ali na Mhe. Soud Mohammed Jumah wameshauri kuwe na motisha kwa wanaoshughulika na ukusanyaji wa taka.

Halikadhalika, wameshauri viwanda vya vinywaji viwe na mifumo ya kurejeleza chupa ili kupunguza hali ya kuzagaa ovyo mitaani na ksuababisha uchafuzi wa mazingira.

Sanjari na hilo, vilevile kamati hiyo imependekeza kuwa madampo ya kisasa yajengwe katika kila wilaya nchini kwani taka zimekuwa zikizalishwa kwa wingi.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila amesema ni kweli kuna changamoto ya uchakavu wa magari ya kubeba taka katika halmashauri.

Kutokana na hali amesema ipo haja sasa kwa halmashauri kuweka vigezo kwa wakandarasi wanaoomba zabuni ya kukusanya taka wawe na magari yenye sifa za ubora.

mipan

Settings