Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Witara aiagiza Manispaa ya Morogoro kujenga dampo la kisasa


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Witara ameiagiza Halmashauri ya Morogoro kujenga dampo la kisasa katika eneo lingine na kuweka usimamizi mzuri wa taka.

Waitara alitoa agizo hilo mara baada ya kutembelea dampo eneo la Viwandani katika Manispaa hiyo na kukuta hali ya usimamizi wa taka isiyoridhisha wakati alipofanya ziara ya mkoani Morogoro kwa lengo la kukagua usimamizi wa mazingira.

Alisema hali katika dampo hilo si nzuri kutokana na kutokidhi vigezo la dampo vikiwemo kutokuwa na utaratibu wa kutenganisha aina za taka ili kuwa na usimamizi mzuri.

“Hapa hakuna usimamizi mzuri hatuwezi kuwa na dampo la aina hii na ni ngumu control taka hapa kama mlivyosema mmetenga eneo la ekari 174 nawahimiza muandike andiko mpate fedha mjenge dampo la kisasa hapa hapafai na si rafiki kwa mazingira haya maji yakisambaa ni hatari kwa binadamu, wanyama na mazingira,” alitadharisha.

Pia naibu waziri huyo alisisitiza elimu itolewe hususan kwa vijana kutumia fursa ya kutumia taka zinazooza ili waweze kujiajiri kwa kutengeneza mbolea ya mboji kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na bidhaa zingine.

Awali akizungumza katika kikao na maafisa mazingira wa mkoa, manispaa na kata za, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waitara alielekeza kila shule ya msingi na sekondari kusimamia kila mwanafunzi apande mti.

“Naelekeza wakurugenzi wote wa wilaya na watu wa mazingira kwenye mikoa na wilaya kuhakiksha kila mwanafunzi anapanda mti, kwa wa shule msingi autunze kwa miaka saba na kwa yule wa sekondari atautunza kwa miaka minne awapo shule hili litasaidia katika si tu katika kutunza mazingira bali pia kupata vivuli na matunda,” alisema.

Aidha, Waitara aliwataka maafisa mazingira kuzitembelea klabu za mazingira zilizopo katika shule mbalimbali ili kutoa hamasa kwa wanafunzi wanaounda klabu hizo kuendelea kushiriki katika utunzaji mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa alisema mikakati iliyowekwa wilayani humo ni kuelekeza kila mwanafunzi anayeanza shule akishirikiana na mzazi wake kupanda mti mmoja na kuutunza.

Msulwa alisema kuwa kwa wastani kila shule inapokea wanafunzi takriban 200 na hivyo wanaamini watapata idadi hiyo ya miti na kuwa kwa kufanya hivyo watasaidia kampeni ya kupanda miti kushika kasi.