Habari
Waziri Masauni aanza ziara Morogoro kukagua maandalizi kukabili El Niño
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameanza ziara mkoani Morogoro ya kukagua hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na mvua za El Niño kwa ajili kubaini mapema maeneo na miundombinu hatarishi ili hatua zichukuliwe kabla ya mvua kubwa kunyesha.
Mhandisi Masauni, amesema ziara hiyo ya siku mbili, Septemba 28 hadi 29, 2026 atakagua na kuangalia mifereji, makaravati, madaraja na njia za maji kama zipo katika hali inayoweza kupitisha maji kwa usalama, huku wananchi wanaoishi maeneo ya mabonde na kando ya mito wakipatiwa taarifa na tahadhari kwa wakati.
Amesema vyombo vya habari vinapaswa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu El Niño ili jamii ichukue hatua kabla ya mvua hizo kufika.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema mkoa huo umeendelea kuhakikisha unachukua hatua za haraka kutokana na jeografia ya mkoa huo kwa kuagua maeneo hatarisha ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbaliikiqemo vyombo vua habari.
“Morogoro ni miongoni mwa mikoa inayoweza kukabiliwa na mafuriko kutokana na uwepo wa mito, mabonde na maeneo ya chini, hali inayofanya maandalizi ya mapema kuwa muhimu katika kulinda maisha, mali, mazao na miundombinu,” amesema Kilakala.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Edina Katalaiya, amesema Mkoa umeandaa mpango wa kukabiliana na athari za El Niño, ukiweka mkazo katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wakati, utambuzi wa maeneo hatarishi na maandalizi ya maeneo ya kuwahifadhi wananchi watakaoweza kuathirika.
Amesema mkoa pia unaendelea kusafisha mito, mifereji, makaravati na madaraja ili kuondoa vizuizi vinavyoweza kusababisha maji kuziba njia na kuleta mafuriko.
Edina amesema maeneo hatarishi katika halmashauri yanaainishwa, huku viongozi wa kata, vijiji, mitaa na kamati za maafa wakipewa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kutambua viashiria vya El Niño.
“ Tunaendelea kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha, vifaa, dawa na vifaa tiba, pamoja na kuandaa timu za uokoaji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi endapo mafuriko yatatokea,” amesema.
Kwa mujibu wa mpango huo, amesema taarifa za TMA zitaendelea kufikishwa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, viongozi wa Serikali za Mitaa, viongozi wa dini na wadau wengine.



