Habari
Tanzan ia mwenyeji Mkutano wa Kimataifa wa Ufugaji Viumbe maji
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Ufugaji Viumbe Maji (International Aquaculture Conference) utakaofanyika Desemba 1 hadi 4, 2026, jijini Dar es Salaam. Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Maduhu Kazi, wakati akifungua Kikao cha Tano cha Kamati Elekezi ya Programu ya Uchumi wa Buluu ya Umoja wa Ulaya, jijini Dar es Salaam, Novemba 12, 2026.
Dkt. Kazi amesema Uchumi wa Buluu ni fursa muhimu kwa maendeleo ya taifa kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira, kuvutia uwekezaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya pwani.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha sekta hiyo kupitia majukwaa ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) na Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesema Tanzania iliendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda mazingira ya bahari na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ushiriki wake katika Mkutano wa 11 wa Our Ocean uliofanyika Mombasa, Kenya, Juni 2026.
Akizungumzia programu hiyo, Dkt. Kazi amesema ina uwekezaji wa Euro milioni 110 kutoka Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake, ikiwa na lengo la kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na pwani, kukuza ajira na kuboresha maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali hizo.
Amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wake, Euro milioni 15.5 zimetolewa kupitia ufadhili wa moja kwa moja wa sekta, huku miradi mitano ya ziada ikiwa imeingia mikataba yenye thamani ya Euro milioni 40.25. Miradi mingine yenye thamani ya Euro milioni 32.6 ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi.
Amehimiza washirika wa utekelezaji kuongeza kasi ya shughuli zao ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinageuka kuwa matokeo halisi kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, Umoja wa Ulaya na wadau wengine wa maendeleo.



