Habari
Masauni aipa kongole NCMC, CRDB kwa kuchochea solo la biashara ya kaboni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, amepongeza Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na Benki ya CRDB PLC kwa kuingia makubaliano ya ushirikiano yatakayochochea ukuaji wa soko la kaboni nchini na kuvutia uwekezaji wa kijani.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) iliyofanyika jijini Antalya, Uturuki, Mhe. Masauni amesisitiza kuwa biashara ya kaboni nchini lazima ilete manufaa halisi ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa Watanzania, ikiwemo ajira, maisha bora, uhamishaji wa teknolojia na uwezeshaji wa jamii za wenyeji.
Amesema ushirikiano huo unaunganisha utaalamu wa NCMC katika kuratibu na kusimamia biashara ya kaboni na uwezo wa CRDB katika huduma za kifedha na uwekezaji, hivyo kuweka mazingira bora ya kufadhili na kutekeleza miradi ya kaboni inayostahili.
Aidha, ameitaka CRDB kuendelea kubuni suluhisho bunifu za kifedha zitakazowezesha upatikanaji wa mitaji kwa waandaji wa miradi ya kaboni na wadau wengine wa soko hilo.
Mhe. Masauni amesisitiza kuwa miradi yote ya kaboni lazima izingatie Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Biashara ya Kaboni), 2022, pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2023, huku akibainisha kuwa upatikanaji wa fedha siyo kibali cha kuanza utekelezaji wa mradi bila kufuata taratibu za kisheria na kupata idhini za mamlaka husika.
Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kitaasisi na udhibiti ili kuhakikisha biashara ya kaboni inakuwa na uwazi, uwajibikaji, uadilifu wa kimazingira na manufaa jumuishi kwa Taifa na wananchi wake.



