Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

​Waziri Jafo atua NEMC, aahidi kukutana na wawekezaji nchini kusikiliza kero zao kuhusiana na uchelewaji wa vibali vya EIA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo, ameahidi kukutana na wawekezaji wote nchini Aprili 17, 2021 ili kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wakati wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), mkutano huo utafanyika Millenium Tower Jijini Dar es Salaam.

Ameyasema hayo alipofanya ziara katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Makao Makuu Mikocheni Jijini Dar es Salaam baada ya uteuzi, akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Hamad Hassan Chande, amesema kuwa kuna malalamiko mengi ameyapata baada ya kuteuliwa juu ya NEMC hasa kwenye mchakato wa utoaji wa Cheti cha EIA.

“Nimeitisha mkutano huu kutokana na malalamiko ya wawekezaji wengi kulalamikia NEMC ndio chanzo cha ucheleweshwaji wa vibali, hivyo kupelekea wawekezaji kushindwa kufanya uwekezaji katika Taifa letu. Hili suala linaathari yake kama mwekezaji anaposhindwa kupata cheti kwa wakati huenda akashindwa kuwekeza kiwanda hapa na kwenda kuwekeza Nchi nyingine na Taifa kupata hasara. Lakini pia lengo langu nataka kufahamu chanzo cha ucheleweshwaji huo,” amesema Mhe. Jafo

Ameendelea kusema kuwa kuna kampeni ya kuhusu mazingira ambayo itazinduliwa rasmi tarehe sita Juni, mwaka huu ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango, amesema kuwa kampeni hii itakuwa kubwa na itahusisha kila Mtu ndani ya Tanzania ili Nchi yetu iwe bora na kila mtu aitamani kwa kuwa na mazingira bora na safi.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Mkamu wa Rais Mhe. Hamad Chande, ametoa shukrani za dhati kwa mapokezi waliyoyapata ofisi hapo na amewaomba ushikamano huu uendelee ili kuweza kufikia malengo kwa maslai ya Taifa. Pia ameeleza kuwa kuna haja ya kutafuta namna ili kufanya mchakato wa utoaji cheti uwe rahisi kuepusha malalamiko kwa wawekezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka, amesema kuwa amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Jafo kuhusiana na kampeni ya usafi na mazingira ambayo itafanyika Nchi nzimana kuhusisha Taasisi na vyombo vya Serikali kwa lengo la kuboresha ustawi wa mazingira

“Suala hili tumelipokea kwa furaha kwani tumekuwa na changamoto kubwa sana zinazohusiana na uchafuzi wa mazingira hasa katika maeneo ya misitu kumekuwa na ukataji mkubwa wa miti, lakini pia mito yetu imekuwa ikichafuliwa kwasababu ya maendeleo ya ukulima pamoja na viwanda ambavyo vinatiririsha maji yasio salama katika mazingira yetu. Mashindano hayo yataleta uamsho katika akili na utendaji mzima wa serikali na watu binafsi na kuona kumbe mazingira ni muhimili mkubwa katika Maisha ya mwanadamu” alisema Dkt. Gwamaka

Dkt. Muhandisi Gwamaka ameendelea kusema kuwa mashindano hayo yataongeza viwango vikubwa vya watu kuweza kuzingatia usafi na utunzaji wa mazingira pasipo kulazimishwa. Hata hivyo itasaidia kupanua uelewa na elimu kwa wadau mbalimbali wa mazingira na Nchi yetu itaendelea kuwa Nchi nzuri yenye mazingira mazuri na watu wenye afya nzuri.

Waziri Jafo amemaliza kwa kuwataka wenye viwanda na wawekezaji wengine kuzingatia sheria ya mazingira ili kuepusha uchafuzi wa mazingira na faini zisizo za lazima. Ameahidi kufatilia viwanda mbalimbali na kuhakikisha wanazingatika sheria bila shuruti. Waziri Jafo akiwa katika ziara yake ofisi za NEMC ametembelea ofisi za watumishi wa Baraza na kusisitiza kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo ili kufikia malengo ya Baraza.