Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

​Waziri Jafo atoa miezi sita kwa machinjio ya Kizota, Dodoma yakamilishe mfumo wa kutibu majitaka


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo ameupa uongozi wa machinjio ya kisasa ya Kizota jijini Dodoma miezi sita kurekebisha changamoto ya utiririshaji wa majitaka ovyo.

Jafo ametoa agizo hilo leo Aprili 8, 2021 alipofanya ziara ya kikazi katika machinjo hiyo kwa ajili ya kukagua udhibiti wa majitaka na utunzaji wa mazingira kwa ujumla.

Alisema kuwa kila kiwanda lazima kiwe na mpango wa namna ya kuyatibu majitaka na kudhibiti utiririshaji wake kuepusha yasiende kwenye makazi yao watu na kusababisha madhara ya kiafya.

“Nafahamu machinjio hii ni miongoni mwa machinjo kubwa na ina soko kubwa katika nchi za Mashariki ya Kati wananunua nyama nami nimekuja hapa kujiridhisha kuhusu suala zima la utiririshaji wa majitaka,” alisema.

Alimuelekeza Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) Kanda ya Kati Flanklin Rwezimula kufuatilia kazi ya kuhakikisha machinjio hiyo inatengeneza mfumo wa kutibu majitaka haraka.

Kwa upande wake Meneja wa machinjio hayo ya Mkoa wa Dodoma ambayo yanasimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Chacha Mwita alisema wameyapokea maelekezo ya Serikali na wanatarajia kukarabati miundombinu hiyo.

Alisema upo mpango wa kuwaogeza baadhi ya wakazi wa eneo la jirani na machinjio hiyo ili waweze kupata eneo la kuhifadhi na kutibu majitaka kupeusha kuyafikia makazi.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo alitembela kiwanda cha kurejeleza taka za plastiki cha Future Colorful Limited kilichopo eneo hilo la Kizota jijini Dodoma na kupongeza juhudi za kiwanda hicho katika kutunza mazingira.

Alitoa rai kwa Wang Zuo Min kuwasiliana na NEMC pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili apewe viwango kwa ajili ya kuzalisha mifuko mbadala.

Awali katika maelezo yake mmiliki huyo alisema kuwa aliachana na biashara ya kutengeneza mifuko ya plastiki baada ya kupigwa marufu na Serikali na hivyo kuomba atumie mitambo yake kuzalisha mifuko mbadala.