Waitara: Wananchi msijenge maeneo yaliyoyotengwa kwa ajili ya viwanda

Mar, 16 2021

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara amewataka wananchi kujiridhisha na maeneo wanayotaka kununua kwa ajili ya makazi ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

Waitara ametoa kauli hiyo leo alipotembelea kiwanda kinachotengeneza nondo cha Fujian Hexingwa Co. Limited kilichopo Kisemvule wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wananchi wakilalamikia uchafuzi wa mazingira hususani moshi unaotoka katika baadhi ya viwanda vinavyozunguka makazi ya watu ikiwemo kiwanda cha Fujian.

“Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda yawe ya viwanda sasa wananchi wakivamia maeneo haya inakuwa kichaka cha malalamiko na kutaka kulipwa fidia, Idara za Mipango Miji zielimishe wananchi kuhusu maeneo hayo yametengwa kwa shughuli gani badala ya kuwaacha wajenge halafu waje kulalamika”.

“Kama ikitokea mtu ameingilia kiwanda akilalamika hatutamsikiliza, mtu lazima ajiridhishe je ni kihalali? Kitu gani kimepangwa kujengwa katika eneo hilo,” alisisitiza Waitara.

Aidha Naibu Waziri huyo aliwataka wamiliki wa viwanda kuajiri wataalam wa mazingira ili waweze kushauri wenye viwanda kuzingatia taratibu kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.

Katika hatua nyingine, aliagiza Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Filberto Sanga asimamie wananchi waliojenga kando ya kiwanda hicho watakapolipwa fidia ifikapo Machi 30 mwaka huu, wawe wameondoka katika eneo hilo ili waondokane na kelele zitokanazo na shughuli zinazofanyika kiwandani hapo.

Vile vile, Naibu Waziri huyo aliwaagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika kiwanda hicho ili kuhakikisha kuwa kinazingatia Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 ili kupunguza uchafuzi wa mazingira utakao weza kujitokeza.

Kwa upande wake Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alisema kuwa malalamiko ya wananchi yanatokana na baadhi ya wananchi kununua viwanja kiholela ambavyo havijapimwa na Halmashauri ya Wilaya na viko karibu na maeneo ya viwanda.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwaelekeza wataalamu wa ardhi na mipango miji kutoka wilaya hiyo kuanza kutenga na kupima maeneo yatakayotumika kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda wilayani humo.

Sanga alimshukuru Naibu Waziri Waitara kwa kufanya ziara ya kutembelea wilaya hiyo hususan katika kiwanda hicho ili kujionea changamoto za kimazingira kwa wananchi wanazonguka kiwanda hicho.

Kiwanda cha Fujian Hexingwa Co. Limited kinalalamikiwa na baadhi ya wananchi kuwa kinatoa moshi mzito pamoja kelele hali inayoathiri mazingira na afya za wakazi waishio karibu na kiwanda hicho.

Settings