Waitara aipa maelekezo NEMC kutatua kuongezeka kina maziwa Singida

Feb, 15 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamzi wa Mazingira (NEMC) kufanya utafiti kuangalia namna ya kudhibiti kuongezeka kwa kina cha maji ya maziwa mkoani Singida.

Ameliagiza Baraza hilo kufanya tathmini na kutoa suluhisho la kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Masogweda na Mulya katika manispaa na wilaya ya Singida ambayo yamefurika na kuleta madhara katika makazi na mashamba.

Waitara alitoa agizo hilo jana wakati wa ziara ya kikazi mkoani humo baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Pasacas Mulagiri ambaye aliomba zichukuliwe hatua kukabiliana na hali hiyo.

Pasacas alionesha hofu ya kumezwa na maji kwa vijiji viwili kutokana na kufurika kwa maziwa hayo mawili na kumuomba Naibu Waziri huyo kulifanyia kazi suala hiyo katika ngazi ya kitaifa.

Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine Waitara alitembelea machinjio katika manispaa hiyo na kuitaka halmashauri hiyo kuharakisha mpango wa kuihamishia eneo lingine walilotenga.

“Niwapongeze viongozi wa manispaa ya Singida nimesikia hapa mna mpango wa kujenga machinjo nyingine kwani baada ya hii na nina imani itakuwa ya kisasa na itakidhi mahitaji maana sasa hivi ninyi ni manispaa na mnahitaji eneo kubwa kuliko hili,” alisema.

Pia katika ziara hiyo alitembelea soko kuu na kuridhishwa na hali ya miundombinu ya kuhifadhi taka ngumu pamoja na dampo lililopo katika eneo la Manga nje kidogo ya manispaa hiyo.

Akizungumza katika kikao na maafisa mazingira kutoka manispaa hiyo Waitara alisema ipo haya ya kuwashirikisha wananchi katika maeneo yao katika masuala ya kuhifadhi mazingira ili kupata taarifa kutoka kwenye vijiji ngazi ya chini.

Naibu Waziri Waitara yuko katika ziara mikoa mbalimbali kwa lengo la kuhimiza uzingatiaji wa Sheria ya Mazingra ya mwaka 2004 na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira hususan upandaji na utunzaji wa miti kwa kila halmashauri.

Settings