Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Usimamizi mbovu wa dampo la Dodoma wamchefua Waziri Jafo, ashusha rungu kwa Wakurugenzi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akitoa maelekezo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye dampo la Chidaya jijini Dodoma ambapo amempa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma mwezi mmoja kujenga ukuta wa kudhibiti majitaka yanayomwagwa hapo.

Jafo ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kushtukiza na kubaini usimamizi usioridhisha katika dampo hilo, jambo linaloweza kuhatarisha afya za wananchi endapo maji hayo yatatiririka kwenye vyanzo vya maji.

Alisema Serikali imetumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya madampo ya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini lakini kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi.

“Hili dampo mmejenga kwa gharama lakini mna usimamizi dhaifu hapa mvua ikinyesha maji yanatatirika kwenda kule bondeni yataingia kwenye ule mto na watu watatumia hayo maji na kuhatarisha afya nyie watu wa site mmeshindwa kabisa hata kusimamia hapa,” alishangazwa.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri ambazo kumejengwa madampo ya kisasa kuimarisha usimamizi wake kwakuwa Serikali imetumia fedha nyingi kuyajenga.

Waziri Jafo, amesema kuwa usimamizi katika Dampo la kisasa la Chidaya kwa uogozi wa jiji la Dodoma, unahitajika ili kusaidia kuimarisha afya za wananchi wanaoishi katika maeneo jirani.

Pia aligiza majitaka yaliyopo katika eneo la dampo hilo yapimwe ili kuweza kubaini yana kiasi gani cha sumu kisha wayatibu kwani yakitiririka yanaweza kutumika na kuhatarisha afya za wananchi.

Katika ziara hiyo akiwa ameambatana na Afisa Mipango Miji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Hussein Omar na Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) Kanda ya Kati Flanklin Rwezimula.