Habari
UNDP yaahidi kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Rais
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesema litaendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais ili kufanikisha utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za masuala ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa Septemba 30, 2026 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo hapa nchini, Bw. Shigeki Komatsubara wakati wa mazungumzo baina yake na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi.
Katika mazungumzo viongozi hao walijadiliana kuhusu vipaumbele vya ushirikiano vinavyohitaji kuwekewa mkazo katika maeneo ya utekelezaji.
Dkt. Muyungi amesema Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa UNDP katika kuwezesha miradi na programu mbalimbali za masuala ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo utekelezaji wa mchango wa taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi (NDC) awamu ya tatu.
Katika kikao hicho Dkt. Muyungi alibainisha maeneo ya kipaumbele katika ushirikiano na shirika hilo ni pamoja na kuomba UNDP kuwezesha Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP 12) unaotarajia kufanyika nchini kuanzia tarehe 6-9 Oktoba mwaka huu.
Amebainisha maeneo mengine ya kipaumbele yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kuwezesha utekelezaji wa mpango wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa programu za kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
“Kipaumbele kingine tulichojadiliana ni pamoja na kuiwezesha Tanzania kuendelea kupata fedha za utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la fedha la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF)” amesema Dkt. Muyungi.
Kwa upande, Bw. Shigeki Komatsubara amesema Shirika hilo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi inayolenga kuleta maendeleo endelevu.
Amesema UNDP na Ofisi ya Makamu wa Rais zimekuwa zikishirikiana katika kufanikisha miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira ambayo ipo katika hatua mbalimbali na hivyo kuhitaji ufutiliaji wa karibu ili kuimarisha utekelezaji wake.
Aidha Bw. Komutsubara amesema miradi na programu hizo ni pamoja na andiko dhana la mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika usimamizi wa taka, mradi wa mchango wa taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi awamu ya tatu, mfuko wa fidia na hasara katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya vyema katika utekelezaji wa programu na miradi ya uhifadhi wa mazingira, hiyo ni hatua nzuri ya kuhakikisha jamii inaendelea kunufaika na mchango wa mazingira ya kimataifa ikiwemo UNDP” amesema Komatsubara.
Viongozi hao pia walikubaliana kuunda timu ya pamoja ya watalaamu itakayohakikisha makubaliano na majadiliano mbalimbali baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na UNDP yanasimamiwa na kutekelezwa ili kufikia malengo ya Dira 2050.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) nchini Tanzania, Bi. Clara Makenya.



