Habari
Tanzania yatoa wito kwa mataifa ya Bahari ya Hindi kuunganisha nguvu kulinda utajiri wa dola bilioni 300
Tanzania iimetoa wito kwa Mataifa ya ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kimazingira katika kulinda rasilimali za bahari zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 300 za Marekani, ikionya kuwa mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hizo yanatishia mustakabali wa uchumi wa buluu na maisha ya mamilioni ya wananchi wanaotegemea bahari kwa chakula na kipato.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, (JNICC) Dar es Salaam.
Akisisitiza umuhimu wa kutafsiri makubaliano ya kimazingira katika hatua madhubuti za kisera, kisheria na kibajeti, Makamu wa Rais amezitaka nchi wanachama kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa buluu unaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na mgawanyo wa haki wa manufaa yatokanayo na rasilimali za bahari.
“Uchumi endelevu wa buluu si kuongeza shughuli za kiuchumi baharini pekee. Ni lazima ulinde mifumo ya ikolojia, utengeneze ajira zenye staha na kuhakikisha manufaa yake yanagawanywa kwa haki,” amesema Mhe. Ndejembi, akisisitiza kuwa uhifadhi na maendeleo vinapaswa kwenda pamoja.
Akieleza umuhimu wa kiuchumi wa bahari hiyo, Makamu wa Rais amebainisha kuwa ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi unazalisha takribani dola bilioni 20.8 kila mwaka, huku huduma za mifumo yake ya ikolojia zikiwa na thamani ya dola bilioni 25 kwa mwaka na utalii ukichangia zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji huo. Zaidi ya watu milioni 65 wanategemea bahari moja kwa moja kwa maisha yao, wakati asilimia 90 ya biashara ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hupitia bandarini, hali inayoifanya bahari kuwa mhimili muhimu wa biashara, ajira, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi ya kikanda.
Hata hivyo, utajiri huo unakabiliwa na tishio kubwa la mabadiliko ya tabianchi, huku joto la uso wa bahari katika ukanda huo likiongezeka kwa wastani wa nyuzi joto 0.1 kila muongo, na kuchangia kupauka kwa matumbawe, kupanda kwa kina cha bahari na mmomonyoko wa pwani unaohatarisha miundombinu na maeneo ya kilimo. Ukanda huo una zaidi ya asilimia 30 ya mifumo muhimu ya matumbawe, mikoko na nyasi bahari duniani, huku mifumo ya ikolojia inayohifadhi kaboni ya buluu ikikadiriwa kuwa na tani milioni 400 za kaboni.
“Mabadiliko ya tabianchi ndiyo tishio kubwa zaidi kwa bahari yetu na jamii za pwani. Ni lazima tuchukue hatua za haraka na zenye dhamira kubwa ili kujenga ustahimilivu na kulinda mifumo ya ikolojia inayotutegemeza,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Kwa upande wa Tanzania, Mh. Ndejembi ameeleza kuwa Serikali imeweka uchumi wa buluu, uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali kuwa sehemu ya msingi ya mageuzi ya kiuchumi kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Tanzania, yenye ukanda wa pwani wa takribani kilomita 1,424, eneo la bahari ya mipaka lenye kilomita za mraba 64,000 na Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bahari wenye kilomita za mraba 223,000, imeimarisha mwelekeo huo kupitia Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Sera ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar ya mwaka 2020, zinazolenga kuchochea maendeleo ya uvuvi, utalii, usafirishaji wa baharini na uwekezaji bila kuhatarisha mazingira.
Katika kuonesha uhusiano kati ya uhifadhi na maendeleo ya kiuchumi, Makamu wa Rais amebainisha kuwa kila dola moja inayowekezwa katika urejeshaji wa mikoko inaweza kuleta manufaa yenye thamani ya dola tano hadi 10 kupitia ulinzi wa pwani, uvuvi na biashara ya kaboni, huku uzoefu wa Zanzibar ukionesha kuwa uwekezaji katika uchumi wa buluu unaweza kuleta manufaa yenye thamani ya mara tano ya fedha zilizowekezwa. Tanzania ina zaidi ya hekta 158,000 za mikoko, huku zaidi ya hekta 3,000 zikiwa zimerejeshwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya Mkataba wa Nairobi, hatua inayodhihirisha umuhimu wa uhifadhi katika kulinda uchumi na ustawi wa jamii za pwani.
Katika kuendeleza fursa hizo, Tanzania inaendelea kuimarisha hifadhi za bahari, kupambana na uvuvi haramu na usioripotiwa, kukuza ufugaji wa viumbe vya majini, utalii endelevu na biashara ya kaboni. Aidha, zaidi ya dola milioni 41 za Marekani zinawekezwa Zanzibar kupitia Mradi wa Kuimarisha Usimamizi Endelevu wa Uvuvi wa Baharini na Ufugaji wa Viumbe vya Majini (TASFAM), unaolenga kuwanufaisha wananchi takribani 160,000 katika kipindi cha miaka mitano, asilimia 80 wakiwa wanawake, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wao katika fursa za uchumi wa buluu.
Akizungumzia mustakabali wa Mkataba wa Nairobi, Makamu wa Rais ameainisha vipaumbele sita vya kuongoza hatua za kikanda, vikiwemo kuimarisha utekelezaji wa makubaliano kupitia sheria, taasisi na bajeti za kitaifa, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kurejesha mikoko, matumbawe na nyasi bahari, pamoja na kudhibiti uchafuzi unaotokana na plastiki, kemikali na maji machafu.
“Ahadi zetu zinahitaji majukumu yaliyo wazi na taarifa za utekelezaji zinazoweza kupimwa. Hili linahitaji utashi wa kisiasa, uwezo wa taasisi na rasilimali za kutosha,” amesema, akizitaka nchi wanachama kuimarisha mifumo ya utekelezaji na kutoa taarifa za maendeleo na changamoto zinazojitokeza.
Katika vipaumbele vingine, ametaka kuimarishwa kwa uhifadhi wa bioanuai na usimamizi wa matumizi ya maeneo ya bahari ili uwekezaji katika uvuvi, bandari, utalii na nishati usihatarishe mifumo ya ikolojia, sambamba na kufikia lengo la kimataifa la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya bahari na pwani ifikapo mwaka 2030. Pia amehimiza uwekezaji katika tafiti za kisayansi, takwimu za pamoja, teknolojia, akili unde na mifumo endelevu ya fedha, pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi, wanawake na vijana katika maamuzi na fursa za uchumi wa buluu.
Makamu wa Rais amepongeza hatua ya COP12 kuanzisha kwa mara ya kwanza Jukwaa la Biashara, Jukwaa la Vijana na ushiriki maalumu wa wanawake, akitaka utaratibu huo kuwa sehemu ya kudumu ya mikutano ijayo. “Wanawake na vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha uchumi huu unakuwa endelevu,” amesisitiza, huku akitaka ushirikiano na sekta binafsi kuzingatia uwajibikaji, ushahidi wa kisayansi na maslahi ya umma, huku akizitaka nchi wanachama kuhakikisha maamuzi ya COP12 yanatekelezeka, yanatengewa fedha na yanaweza kupimwa matokeo yake, kwa kuwa changamoto za uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa makazi ya viumbe hai hazitambui mipaka ya kitaifa.
Akihimiza hatua mpya za ushirikiano wa kikanda, Mhe. Ndejembi amesema maadhimisho ya miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi yanapaswa kuwa mwanzo wa mwelekeo mpya wa kulinda bahari na kujenga uchumi imara unaowanufaisha wananchi. “Tufanye maadhimisho haya ya miaka 40 yakumbukwe si kwa kusherehekea yaliyopita pekee, bali kama hatua ya mabadiliko kuelekea bahari yenye afya na jamii zenye ustahimilivu zaidi,” amesema, akisisitiza umuhimu wa mataifa kuunganisha nguvu katika kulinda rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Bi. Elizabeth Maruma Mrema, ameeleza kuwa miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi imeweka msingi imara wa ushirikiano wa kikanda katika uhifadhi wa mifumo ya ikolojia ya bahari, kujenga uaminifu baina ya nchi wanachama na kuimarisha usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari. Kwa mujibu wake, COP12 inatoa fursa kwa mataifa hayo kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na udhibiti ili kukabiliana na changamoto mpya za usimamizi wa bahari, huku tafiti za kisayansi zilizopitiwa na wataalamu na uhifadhi wa makazi muhimu ya viumbe vya baharini vikiwa nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi ya uchumi endelevu wa buluu.
Bi. Mrema pia amehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimkakati baina ya Serikali, Taasisi za Kisayansi, Asasi za Kiraia na Wadau wengine, sambamba na kujenga uwezo wa kitaasisi na kitaalamu ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mipango ya kikanda. Katika suala la uwekezaji, amebainisha kuwa fedha za umma pekee haziwezi kukidhi mahitaji ya kuendeleza uchumi endelevu wa buluu, hivyo kuna ulazima wa kushirikisha taasisi za fedha na wadau wengine wa uwekezaji, huku utashi wa kisiasa na mshikamano wa kikanda vikiwa nguzo muhimu za kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuweka msingi madhubuti wa maendeleo ya bahari kwa miaka ijayo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, ameeleza kuwa COP12 inatoa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kubadilishana maarifa na uzoefu pamoja na kutambua fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za bahari. Mkutano huo, unaohusisha vikao vya washirika wa maendeleo na kamati za kitaalamu, unafanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi, huku ukilenga kuweka mwelekeo mpya wa ushirikiano utakaosaidia kuongeza ajira, kulinda mazingira ya bahari na kutumia kikamilifu fursa za bioanuai kwa manufaa ya wananchi, hususan wanawake, vijana na watoto.
Mhandisi Masauni amebainisha kuwa Tanzania imenufaika na ushirikiano chini ya Mkataba wa Nairobi kupitia msaada wa kitaalamu katika usimamizi wa mazingira ya bahari, udhibiti wa uchafuzi na kuimarika kwa ushirikiano na wadau wa kikanda na kimataifa. Amehimiza kuendelezwa kwa mafanikio hayo kupitia ushirikiano wa kimkakati na matumizi endelevu ya fursa za uchumi wa buluu ili kuchochea maendeleo, kuongeza ajira na kulinda rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mkutano huo, unawakutanisha washiriki zaidi ya 1,500 kutoka nchi mbalimbali duniani, zikiwemo nchi 10 wanachama wa Mkataba wa Nairobi, unafanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026, chini ya kaulimbiu inayolenga uchumi endelevu wa buluu kwa manufaa ya watu na mazingira. Mkataba wa Nairobi, uliopitishwa mwaka 1985, unazikutanisha Tanzania, Kenya, Msumbiji, Somalia, Afrika Kusini, Madagascar, Mauritius, Shelisheli, Comoro na Ufaransa, na katika kipindi cha miaka 40 umechangia kuanzishwa kwa hifadhi za bahari, kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kuweka mifumo ya pamoja ya usimamizi wa mazingira ya bahari na pwani.



