Habari
Tanzania yahimiza mshikamano kutetea maslahi ya Afrika
Tanzania imehimiza mshikamano wa mataifa ya Afrika katika kutetea maslahi ya pamoja katika makubaliano ya mkutano wa 31 wa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP 31).
Kauli hiyo imetolewa na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mkutano wa 21 wa Mawaziri wa Mazingira wa Afrika (AMCEN) uliofanyika Novemba 15, 2026 Antalya, Uturuki na kujadili msimamo vipaumbele vya mataifa ya Afrika kuelekea kilele cha Mkutano wa COP 31.
Akizungumza wakati wa mkutano huo,Bi. Kemilembe Mutasa - Mkurugenzi wa Mazingira kwa niaba ya Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi, amesema ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kuonesha msimamo madhubuti unalenga kupaza sauti ya pamoja katika kuhimiza upatikanaji wa fedha, utaalamu na teknolojia ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa kupitia Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi (AGN), Tanzania inapongeza juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika katika kufanikisha majadiliano na makubaliano yanayolenga kutetea maslahi ya pamoja.
Amesema Tanzania imeanisha maeneo muhimu ya kipaumbele kuelekea makubaliano ya mkutano wa COP 31 ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ustahilimu na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, haki za kijamii na kiuchumi katika mabadiliko ya tabianchi na masoko ya biashara ya kaboni.
Aidha amefafanua kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi za pamoja za mataifa ya Afrika zenye malengo ya kujenga uwezo kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vijana ili kuwawezesha kuongoza majadiliano ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
“Tanzania iliendesha mafunzo ya kwanza kwa Vijana 60 kutoka mataifa 15 ya Afrika yaliyofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, hii ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya Mkutano wa Umoja wa Afrika” amesema
AMCEN ni jukwaa la kudumu linalounganisha Mawaziri wa Mazingira kutoka nchi 54 za Afrika ili kuwezesha uratibu na ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira Barani Afrika.



