Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

​Serikali yaweka matumbawe katika mwambao wa pwani


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande amesema Serikali imeanza kuweka matumbawe bandia katika maeneo ya mwambao wa Dar es Salaam, Unguja na Pemba.

Chande amesema hayo leo Septemba 7, 2021 wakati akijibu swali la Mbunge wa Wingwi, Mhe. Omar Issa Kombo aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaweka matumbawe bandia na kupanda mikoko katika bahari ili kurejesha mazalia na makulia ya samaki yaliyoharibika.

Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri alisema katika eneo la Sinda Pwani ya Dar es Salaam eneo la mita za mraba 2000 limepandikizwa matumbawe bandia, kwa upande wa Unguja na Pemba matumbawe bandia 90 aina ya reef ball yalipandikizwa katika kijiji cha Jambiani na matumbawe bandia 46 na mapande maalum (Layer Cakes) 6 katika kijiji cha Kukuu.

Alibainisha kuwa matumbawe hayo yalifuatiliwa ukuaji wake kitaalamu na matokeo yameonesha mafanikio makubwa kwa kuimarika kwa mazalia ya samaki na hivyo kuongezeka kwa kiwango cha viumbe hao katika maeneo hayo.

Kuhusiana na upandaji wa mikoko, alisema Serikali imekuwa ikiongeza jitihada zaidi katika upandaji wake katika fukwe mbalimbali za nchi nzima kwa kushirikiana na asasi binafsi na washirika wa maendeleo.

“Takribani hekta 7 za mikoko zilipandwa Unguja na hekta 10 zilipandwa Pemba kwa mwaka 2020 hadi 2021 na upandaji wa hekta 13.5 unaendelea mpaka sasa na matarajio ni kupanda hekta 15 kwa mwaka huu,” alisema Chande.

Aidha, kwa upande wa Tanzania Naibu Waziri alisema hekta 105 zimepandwa katika Delta ya Rufiji huku matarajio ni kupanda hekta 2000 kwa pwani yote ya Tanzania bara ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.

“Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatunza, tunahifadhi, na kusimamia matumbawe na mikoko, pamoja na mifumo ikolojia inayopatikana ndani ya bahari yetu,” alisema.