Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Makamu wa Rais

Serikali: Tulinde Tabaka la Ozoni

Sep, 14 2026

Serikali imewataka Watanzania kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi zinazoharibu Tabaka la Ozoni, ikiwemo majokofu na viyoyozi vilivyotumika, ili kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, katika tamko lake kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni inayoadhimishwa Septemba 16, kila mwaka.

Masauni ametoa wito huo Septemba 14, 2026 Jijini Dar es Salaam akieleza kuwa Tabaka la Ozoni lina umuhimu mkubwa katika kulinda dunia kwa kuchuja sehemu kubwa ya mionzi hatari ya jua kabla haijafika kwenye uso wa dunia.

Amesema uharibifu wa tabaka hilo unaweza kuongeza mionzi ya jua inayofika duniani na kusababisha madhara mbalimbali kwa afya za binadamu na mazingira, yakiwemo saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, kudhoofika kwa kinga ya mwili na kuzeeka kwa ngozi.

Kwa mujibu wa Waziri Masauni, uharibifu wa Tabaka la Ozoni pia unaweza kuathiri ukuaji wa mimea, kuongeza joto duniani na kuchangia mabadiliko ya tabianchi.

“Shughuli mbalimbali za kibinadamu zinachangia kumong’onyoa Tabaka la Ozoni, hasa matumizi ya kemikali zinazotumika katika majokofu na viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji wa chuma, utengenezaji wa magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kilimo cha maua na uhifadhi wa nafaka maghalani”.

Masauni amesema Tanzania itaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha siku hiyo, ambayo huadhimishwa kila Septemba 16 ikiwa ni kumbukumbu ya kutiwa saini kwa Itifaki ya Montreal ya mwaka 1987 kuhusu kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni.

Amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inalenga kuhimiza hatua za kimataifa za kulinda Tabaka la Ozoni na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku ikitambua miaka 10 tangu kupitishwa kwa Marekebisho ya Kigali mwaka 2016.

“Utekelezaji wa Marekebisho haya unaonesha namna ambavyo dunia inaweza kuungana pamoja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za mazingira zinazoendelea kujitokeza,” amesema.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imepanga kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi Tabaka la Ozoni na kuhamasisha matumizi ya kemikali rafiki kwa mazingira.

Aidha, Serikali itatoa mafunzo kwa maafisa forodha na wasimamizi wa sheria kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupitia Bandari Kuu ya Dar es Salaam, pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Masauni ametoa rai kwa wananchi kununua bidhaa zenye nembo rasmi zinazoonesha kuwa ni “Ozone friendly” au zenye “low global warming potential”, yaani bidhaa rafiki kwa Tabaka la Ozoni au zenye uwezo mdogo wa kuchangia ongezeko la joto duniani.

Pia amewataka wananchi kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani na vifaa vya kuzimia moto vyenye kemikali zinazoweza kuharibu Tabaka la Ozoni au kuchangia ongezeko la joto duniani.

Amesema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinafanikiwa.

“Naam kupitia kwenu wanahabari, naamini elimu hii itaendelea kutolewa kwa jamii ya Watanzania ili kuongeza ushiriki wao katika kutekeleza jukumu hili la kulinda sayari hii,” amesema.

Masauni amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulinda Tabaka la Ozoni, akisisitiza kuwa hatua za sasa ni muhimu kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Habari

Settings