Habari
Naibu Waziri Kwagilwa apiga marufuku magari ya Serikali kubeba mkaa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa amepiga marufuku magari ya Serikali kubeba mkaa hatua hiyo inalenga kuongeza jitihada za kuhifadhi mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
Kwagilwa ametoa katazo hilo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha alipomwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Yussuf Masauni, akieleza kuwa kumekuwa na baadhi ya magari ya Serikali yanayobeba mkaa bila kuwekewa vizuizi hali inayokwenda kinyume na jitihada za Serikali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
“Katika mwendelezo huo hatuna budi kuchukua hatua ngumu ngumu kama hizi na katika mwendelezo huo ili tukafikie lengo la mwaka 2034 la watanzania asilimia 80 kuondokana na nishati ambazo zinapelekea kukata miti na kwenda kwenye nishati salama hatuna budi kuchukua hatua ngumu ngumu kama hizi tulizotangaza.” amesema Mhe. Kwagilwa.
Akisisitiza umuhimu wa katazo hilo, Mhe. Kwagilwa amesema uhifadhi na utunzaji wa mazingira ni miongoni mwa nguzo muhimu za Dira ya Taifa hivyo kila taasisi na mwananchi anapaswa kushiriki katika kulinda mazingira na kuunga mkono matumizi ya nishati safi ili kupunguza utegemezi wa nishati zinazochochea ukataji wa miti.



