Naibu Waziri Khamis ahimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia

Jun, 04 2025

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amehimiza wananchi kuendelea kuunga mkono Serikali katika kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Ametoa kauli hiyo wakati akitembelea na kukagua mabanda ya maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 4, 2025 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Mhe. Khamis alisema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia gesi pekee kama ambavyo wengi wanafikiria bali inajumuisha nyenzo zote za kupikia ambazo haziharibu mazingira zikiwemo mkaa mbadala na majiko janja yanayoitumia kiwango kidogo cha umeme.

Alisema Serikali imetatua changamoto ya umeme kwa kutekeleza mradi wa kufua umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere na kusambaza nishati hiyo vijijini ili kuwezesha wananchi wengi kunufaika nayo kwa bei nafuu.

Aidha, alipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuendelea kufunga miundombinu ya gesi katika kambi zao na hivyo kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Akiendelea kutembelea mabanda ya wizara, taasisi na kuzungumza na wadau wa mazingira aliwapongeza kwa juhudi zao za kushirikiana na Serikali katika kusukuma mbele ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Katika hatua nyingine aliwapongeza wadau kwa kubuni mbinu mbalimbali za kusimamia taka zikiwemo kurejeleza taka kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo mbolea.

Mhe. Khamis alisema kuwa hatua hiyo ni mojawapo ya uungaji mkono Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka (2025-2030) ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Settings