Habari
Masauni: Tanzania inaweka mazingira safi ya uwekezaji biashara ya kaboni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Tanzania inaendelea kuweka mazingira safi na salama kwa wadau wenye nia ya kuwekeza kwenye Biashara ya Kaboni hapa nchi.
Mhe. Masauni amesema Tanzania inazidi kujifunza kupitia nchi marafiki ambao wamepiga hatua kwenye Biashara ya Kaboni ili kuendelea kupata mbinu katika eneo hilo.
Ameyasema hayo Mei 18, 2028 jijini Dar es Salaam alipokutana na Ujumbe kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali ya Marekani ya Innovative Sustainable Biotechnologies (ISB) yenye nia ya kuwekeza nchini katika eneo la Biashara ya Kaboni.
Ameongeza kuwa ni muda mwafaka kwa Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Biashara ya Kaboni hasa kila mtu katika eneo analoishi.
Mhe. Masauni amesisitiza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutoa elimu kwa umma hasa kupitia makundi mbalimbali katika Biashara ya Kaboni ili kila mmoja anufaike.
Amesema wananchi wanapaswa kukitumia vyema Kituo cha Taifa cha kuratibu Kaboni (NCMC) kilichopo Mkoa wa Morogoro ili kuweza kupata msaada wa namna ya kujihusisha na Biashara ya Kaboni.



