Habari
Masauni aahidi hatua za haraka kukabiliana na mafuriko mvomero
Serikali imeendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kusikiliza maelekezo ya wataalamu hasa kipindi hiki ambapo jitihada mbalimbali zinafanyika kukabiliana na athari za mvua za El Nino.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi wa Kata ya Muhonda na Sungaji wakati akiwa kwenye ziara Wilaya Mvomero mkoani Morogoro, Septemba 28, 2026.
Mhe. Masauni amesema Serikali inaendelea kupambana kutafuta suluhisho la kudumu hasa kwa wakazi wa kata hizo ambao wamekuwa wakiathirika kila wakati kutokana na kujaa maji kwa Mto Mbulumi.
“Muendeleze Maisha yenu kipindi hiki katika mazingira ya uangalifu, kwa kuwa serikali haipendi kuona mwananchi wake anapata madhara licha ya kwamba mazingira mliyokuwa nayo ni magumi, lakini niwahakikishie kwamba serikali haiwezi kufumbia macho jambo hili.
“Tayari wataalamu wameshaeleza njia ya kutatua tatizo hili na fedha ambazo wamesema, serikali itahakikisha zinapatikana na kuanza kushughulikia jambo hili kwa haraka iwezekanavyo ili wananchi muendelee kuishi kwa amani katika maeneo yenu,” amesema Waziri Masauni.
Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa jambo hili anatarajia kukutana na Waziri wa Maji, TAMISEMI pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kulijadili suala hilo na kulipatia ufumbuzi haraka.
Waziri Masauni amesema pamoja na jitihada ambazo Serikali inachukua kuhakikisha maisha ya wananchi wake yanakuwa salama lakini mafuriko yanapotokea huharibu miundombinu ambayo imetumia fedha nyingi, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa makini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Maulid Dotto amesema pamoja na kuhamashisha wananchi waishio maeneo hatarishi kuhama mapema kabla ya El Nino, jitihada nyingine walizochukua ni pamoja na kushafisha mitaro ya maji, kuondoa takataka na udongo kwenye madaraja na mito.
“Tumerahisha mfumo wa mawasiliano na utoaji wa tahadhari mapema ambapo wilaya imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kila wakati kuanzia ngazi ya vijiji, kata, hadi wilaya,” amesema Mhe. Dotto.
Ameongeza kuwa Kamati za usimamizi wa maafa ngazi ya vijiji na kata zimeelekezwa kuanza na kubainisha maeneo ya kuwahifadhia wahanga pamoja na kufanya tathmini ya upatikanaji wa rasilimali za kuhudumia waathirika kipindi cha El nino.
Amesema mito inayopita katika tarafa za Turiani na Mvomero chanzo chake ni inaanzia mikoa ya Manyara, Dodoma na Tanga na kufanya wilaya hiyo kukumbwa na mafuriko hata kama hakuna mvua ndani ya wilaya hiyo.



