Habari
Makamu wa Rais ashiriki msiba wa mama wa Naibu Waziri Ngwaru Maghembe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi ameshiriki msiba na dua ya kumuombea Bi. Kudra Salim Maghembe, ambaye ni Mama wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe.
Dua hiyo ilifanyika katika makazi ya familia ya marehemu, Wialaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro na kufuatiwa na mazishi yaliyofanyika, Usangi wilayani Mwanga leo tarehe 12 Oktoba 2026.
Katika msiba huo, Makamu wa Rais amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anawaombea faraja wanafamilia pamoja na wananchi wa Mwanga katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Amesema mchango wa Marehemu Bi. Kudra Maghembe ni mkubwa katika kuleta maendeleo ya Wilaya ya Mwanga na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla, kwa kuwa amekua mlezi muhimu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe kwa kumjenga kuwa kiongozi bora, ambaye analitumikia Taifa kwa sasa.
Pia amesema marehemu Bi. Kudra Maghembe alitoa mchango kwa mwenza wake ambaye ni Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Taznania Mhe. Prof. Jumanne Maghembe katika kuwatumikia wananchi wa Mwanga na Taifa kwa ujumla.



