​Makamu wa Rais afungua maonesho ya Sido Kigoma

Sep, 22 2021

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo Septemba 22,2021 amefungua rasmi maonesho ya tatu ya Sido kitaifa yanayofanyika katika uwanja wa Umoja wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Akizungumza katika ufunguzi wa maonesho hayo, Makamu wa Rais bado mchango wa viwanda vidogo katika uchumi wa taifa ni mdogo ikiwemo baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vidogo kutokidhi mahitaji ya wananchi na baadhi kutokidhi mahitaji ya soko. Kufuatia hali hiyo Makamu wa Rais ameielekeza wizara ya Viwanda na Biashara kufanya tathimini ya kina kuhusu Sido juu ya changamoto na mafanikio yake ili kupata mikakati bora itakayopelekea Tanzania kuweza kukidhi mahitaji ya uchumi wa kati.

Kufuatia changamoto ya wajasiriamali kukosa kushindwa kupata mikopo kutoka katika taasisi mbambali za fedha, Makamu wa Rais ameziasa taasisi za fedha kubuni namna bora Zaidi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo kubadili dhamana mbalimbali zinazotumika ili kurahisisha wananchi wengi Zaidi kunufaika na mikopo hiyo. Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Benki na taasisi za kifedha kuendelea kupunguza riba katika mikopo inayotolewa ili kuwasaidia wajasiriamali kuongeza uzalishaji.

Aidha Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Sido kutumia Balozi za Tanzania nje ya nchi katika kupata teknolojia mpya na rafiki pamoja na kujifunza namna taasisi zinazofanana na Sido zinavyofanya kazi katika nchi hizo.

Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi wote kwamba serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogo hapa nchini ziweze kuwa na bei nafuu na kupanua soko lake ili kukuza viwanda vya ndani. Amesema serikali imeweka kipaumbele katika kutekeleza miradi yote ya kimkakati ikiwemo ile ya nishati na miundombinu itakayokuwa chachu kuinua uchumi wa wananchi.

Akiwa katika hadhara hiyo Makamu wa Rais ameiagiza wizara ya nishati pamoja na shirika la umeme nchini Tanesco kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara mkoani Kigoma na maeneo mengine ya nchi. Amemuagiza waziri wa nishati kuhakikisha changamoto ya ukatatikaji wa umeme na usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Kigoma inamaliza kabla ya Oktoba 15 mwaka huu 2021.

Settings