Maafisa mazingira washirikishwe wakati wa utoaji wa vibali

Sep, 16 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande ametoa mwito kwa mamlaka zinazohusika katika utoaji wa vibali vya uwekezaji kuwashirikisha maafisa mazingira kutoka Serikali za Mitaa kuepusha changamoto mbalimbali.

Chande alitoa mwito huo Septemba 16, 2021 wakati akizungumza katika kikao kazi na maafisa mazingira kutoka Halmashauri ya Mji wa Babati na Wilaya ya Babati alipofanya ziara ya kikazi mkoani Manyara.

Alisema kuwa maafisa mazingira wamekuwa hawashirikishwi kikamilifu katika michakato ya kutoa vibali vya ujenzi wa miundombinu ya biashara hatua inayowafanya washindwe kutambua wajibu wao.

“Kuna mtu alinunua eneo kwa ajili ya makazi lakini kinyume chake akabadilisha matumizi na kulifanya kituo cha mafuta, na iligundulika kuwa kumbe maafisa mazingira wala halmashauri zao hawakushirikishwa,” alisema.

“Katika maendeleo bora ya maisha ya mwanadamu ni uwepo wa mazingira kwa sababu mazingira ndio uhai wetu, ndio sehemu ya maisha yetu hivyo ni lazima tuweke mkazo katika utunzaji wa mazingira, pia pamoja na kujali uchumi wetu tusisahau suala zima la utunzaji wa mazingira,” aliongeza.

Aidha, Naibu Waziri Chande alitahadharisha kuhusu athari za kelele kuwa za kiwango kikubwa kutokana na ukuaji wa miji na ambayo husababishwa na uwepo wa fursa kwa wananchi akisema kuwa si jambo baya lakini uwekezaji usikwaze watu wengine.

“Uwekezaji ni mzuri lakini je unawekeza kwa misingi gani na uwekezaji wako hauwakwazi wengine wanaokuzunguka? Hatuwezi kukuangalia wewe mmoja kwa maslahi yako ukawa unaangamiza ama unateketeza wananchi walio wengi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Chande ametembelea kiwanda cha sukari cha Manyara kilichopo wilayani Babati kwa ajili ya ambapo amewapongeza kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira pamoja na kutengeneza mkaa mbadala kutokana na makapi ya miwa.

Alitoa wito kwa uongozi wa kiwanda hicho kusambaza nishati hiyo mbadala inayozalishwa kiwandani hapo kwa wananchi na kwa bei nafuu ili kusaidia kupunguza ukataji holela wa miti.

Hata hivyo kwa upande wake Meneja Kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bw. Lewis Nzali pamoja na pongezi kwa kiwanda hicho, alibainisha baadhi ya changamoto zikiwemo ukosefu wa vifaa kinga kwa wafanyakazi na wageni wanaotembelea hali inayoweza kusababisha athari za kiafya.

Alionesha wasiwasi kutokana na mvuke wenye joto kali unaotoka wakati wafanyakazi hao wakiwa kazini ambapo alishauri itafutwe namna bora ya kupunguza muda wa kukaa katika joto.

Pia alishauri kiwanda aajiriwe mtaalamu wa mazingira na usalama katika kiwanda ili kuwashauri nini cha kufanya ili kulinda mazingira na usalama wa wafanyakazi kwa ujumla.

Awali akitoa taarifa, Afisa Uhusiano wa kiwanda hicho, Bw. John Geu alisema kwa vile miwa hutumia maji mengi katika uzalishaji wanatumia maji ya visima badala ya mto ambao ni chanzo kikuu cha maji. Aliongeza kuwa katika kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi mazingira wamepanda miti pembezoni mwa mto .

Settings