Jafo akipa siku 45 kiwanda cha NIDA kupata kibali cha kutiritrisha majitaka

Jul, 26 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo ametoa siku 45 kwa Kiwanda cha nguo cha NIDA Textile Industries kuhakikisha kimepata kibali cha kutiririsha maji yanayoingia mtoni kutoka Mamlaka ya Bonde Mto Wami- Ruvu kinachothibitisha usalama wa maji hayo.

Jafo ametoa agizo hilo leo Julai 26, 2021 wakati wa ziara yake kiwandani hapo eneo la Tabata jijini Dar es Salaam ambapo alibaini hakina kibali cha kutiririsha maji kitu ambacho ni muhimu kwasababu kina mfumo wa kutiririsha maji taka.

"Ninatoa siku 45 ikiwa na maana ya mwezi mmoja na nusu muwe mmeshapata kibali kutoka Mamlaka ya Bonde kuhusiana na maji taka mnayotiririsha kama ni salama au la mana maji haya hayaonyeshi kwa macho maji haya ni salama kwa mazingira na

viumbe hai," alisema.

Pia, Jafo alitembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha Royal Soap and Detergents kilichopo Kata ya Mabibo mkoani humo kujionea changamoto za uchafuzi wa mazingira ukiwemo hewa ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu na wananchi wa eneo hilo.

Akiwa Kiwandani hapo alisikiliza pande zote mbili yaani uongozi wa kiwanda na wananchi uliowakilishwa na Diwani wa kata hiyo, Mhe. Joseph Kleruu hivyo Waziri jafo alielekeza kifanyike kikao kati ya mwenye kiwanda, Afisa Mazingira wa Manispaa pamoja Diwani na Mwenyekiti wa Mtaa huo baada ya kubaini changamoto ya mahusiano.

“Nimeona kuna changamoto ya kimahusiano katika eneo hili tafadhali wekeni mahusiano mazuri na wananchi wanaowazunguka hiyo ni muhimu naagiza mfanye kikao ndani ya wiki mbili kupata ufumbuzi wa suala hili na ndani ya miezi sita tutakuja tena kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo umefanyika au la,” alisisitiza.

Akizungumza baada ya kupokea maelekezo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kheri James alimhahikishia Waziri Jafo kupokea maagizo hayo na atayafanyia kazi na taarifa ya makubaliano itapelekwa Ofisini kwa Waziri kama alivyoagiza.

Naye Meneja wa Uendeshaji wa Kiwanda hicho, Ntula Shalanda amemuahidi Waziri Jafo kupokea maagizo hayo na kuyafanyia kazi na watakutana na Wawakilishi hao wa wananchi kama alivyoagiza.

Settings