Habari
Dkt Muyungi, BRAC kuimarisha ushirikiano katika hifadhi ya mazingira
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyingi amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania ofisini kwake jijini Dodoma leo Julai 22, 2026.
Lengo la mazungumzo hayo ni kuimarisha ushirikiano na kudumisha mshikamano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilijadili fursa za kupanua ushirikiano katika utekelezaji wa mradi mpya unaojulikana kama BIGBET—programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Programu hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kujenga ustahimilivu na kuwaondoa katika mazingira ya hatari yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania kwa ushirikiano na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika nchi nne, ukiwa na lengo la kuleta matokeo chanya na endelevu kwa jamii zinazolengwa.
Aidha, ujumbe huo uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Joydeep Sinha, akiambatana na Meneja wa Mradi Bw. Jumanne Magese na Naibu Meneja wa Uhamasishaji wa Rasilimali Kelvin Edward.



