Habari
Masauni: COP12 kuimarisha ushirikiano wa kikanda
Tanzania inatarajia kutumia Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) kuimarisha diplomasia yake ya mazingira, kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa, na kuvutia uwekezaji katika Uchumi wa Buluu unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani.
Mkutano huo, unaotarajiwa kuanza Oktoba 6, 2026, jijini Dar es Salaam, utatoa fursa ya kujenga misimamo na hatua za pamoja za kukabiliana na uchafuzi wa bahari, uvuvi haramu, uharibifu wa mifumo ya ikolojia na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akitoa tamko kuhusu maandalizi na matarajio ya mkutano huo Oktoba 4, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema COP12 itakuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wawekezaji na fursa zilizopo katika uvuvi, utalii wa baharini, kilimo cha mwani, uchumi unaotegemea rasilimali za kibaiolojia na huduma za mifumo ya ikolojia.
Amesema Tanzania inalenga kuhakikisha mkutano huo unatoa matokeo yanayotekelezeka katika kulinda mazingira ya bahari na pwani, kuendeleza Uchumi wa Buluu na kuboresha ustawi wa wananchi, hususan jamii zinazotegemea rasilimali hizo kwa maisha na shughuli za kiuchumi.
Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu: **“Towards a Sustainable Blue Economy in the Western Indian Ocean for People and Nature: A 40-Year Journey”**, inayomaanisha **“Kuelekea Uchumi wa Buluu Endelevu katika Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi kwa Manufaa ya Watu na Mazingira ya Asili: Safari ya Miaka 40.”**
Waziri Masauni amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na kwa kuipa kipaumbele sekta ya mazingira, ikiwemo uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.



