Habari
Tanzania yasisitiza nchi za Mkataba wa Nairobi kushirikiana kukomesha uchafuzi wa Bahari
Tanzania imewataka Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuchukua hatua madhubuti na za pamoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa bahari na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za baharini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ametoa wito huo wakati wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), kutoka eneo la Bahari ya Hindi Magharibi ulioanza leo Oktoba 6, 2026, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mhe. Masauni amesema changamoto zinazoikabili bahari zimeongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi, yanayosababisha ongezeko la joto na tindikali katika maji, hali inayotishia miamba ya matumbawe, uvuvi na maisha ya jamii za pwani.
Amesisitiza kuwa uchafuzi wa plastiki na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali vinaendelea kuharibu mifumo ikolojia ya baharini, hivyo maamuzi ya COP12 yanapaswa kujengwa katika ushahidi wa kisayansi na kuelekezwa kwenye utekelezaji wa hatua za kitaifa na kikanda.
Waziri Masauni amesisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii za pwani, wanawake na vijana katika sera na mipango ya uhifadhi, akisema changamoto hizo zinahitaji majibu yanayounganisha uhifadhi wa mazingira, maisha ya wananchi, usalama wa chakula na uchumi wa buluu.
Alisema Tanzania katika kipindi cha uenyekiti wa Mkataba wa Nairobi imesimamia hatua mbalimbali, zikiwamo kukamilishwa kwa Itifaki kuhusu Bioanuai za Baharini na Maeneo ya Pwani na Hifadhi, Mpango wa Kikanda wa Dharura za Mafuta na Mkakati wa Kikanda wa Plastiki na Kemikali Zinazohusiana Nazo.
Aidha, Tanzania imeanza kuandaa Dira ya Kikanda na Mfumo wa Utekelezaji kuhusu Bioanuai za Bahari katika Maeneo ya Nje ya Mamlaka ya Kitaifa (BBNJ), huku baadhi ya nyaraka hizo zikitarajiwa kuwasilishwa kwa ajili ya kupitishwa katika COP12.



