Habari
Kwagilwa ahimiza ushirikiano nchi za Mkataba wa Nairobi
NAIBU Waziri,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuendelea kushirikiana katika kuhifadhi bahari na kutumia kwa pamoja fursa za uchumi wa buluu zinazopatikana katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Kwagilwa ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufungua rasmi mjadala wa Jukwaa la Biashara uliojadili fursa za uwekezaji na biashara kwa ajili ya uchumi endelevu wa buluu katika Bahari ya Hindi ya Magharibi, ikiwa ni siku ya pili ya Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali kujadili fursa za kibiashara na kiuwekezaji katika uchumi wa buluu kwenye ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Alisema jukwaa hilo limewakutanisha wafanyabiashara, wajasiriamali wa kati na wadogo, benki, majukwaa ya kifedha, taasisi za utafiti, taasisi za elimu ya juu pamoja na wavumbuzi, kwa lengo la kujadili namna ya kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu.
“Mimi ujumbe wangu kwa wenzetu, nchi wanachama wenzetu, nafikiri tuendelee kushirikiana,” alisema.
Alisema ushirikiano huo ni muhimu kutokana na ukweli kwamba ikolojia ya bahari pamoja na rasilimali zilizopo baharini zinakwenda nje ya mipaka ya kila nchi.
“Kwa hiyo ni muhimu sisi kama nchi wanachama wote tuendelee kushirikiana ili tuweze kuihifadhi bahari na tuweze kuzitumia fursa za uchumi wa buluu kwa pamoja, kwa kuzingatia kwamba vitu ambavyo viko ndani ya ekolojia ya bahari vinakwenda nje ya mipaka ya kiutawala ya nchi moja,” alisema.
Alisema fursa za uchumi wa buluu zinazojadiliwa katika jukwaa hilo zinahusisha shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Bahari ya Hindi, ikiwemo kilimo, ufugaji, usafirishaji, utalii, michezo na uvuvi.
“Ziko fursa: kwanza fursa za kilimo. Kipo kilimo kinafanyika kwenye ukanda wa bahari kama kilimo cha mwani, utunzaji wa miti kama mikoko, na kilimo cha aina kama hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa shughuli nyingine zinazounda mnyororo wa uchumi wa buluu ni usafirishaji kupitia bandari, meli na vyombo vingine, pamoja na shughuli za utalii na michezo zinazofanyika baharini.
“Lakini ziko shughuli za uchimbaji madini, lakini vilevile utafutaji wa nishati, shughuli za kutafuta fursa za nishati kwenye bahari,” alisema.
Aliongeza kuwa shughuli hizo kwa ujumla wake zinatengeneza mnyororo mpana wa uchumi wa buluu na shughuli za kiuchumi ndani ya bahari, ambazo zimekuwa sehemu ya mjadala katika jukwaa hilo.
Alisema Tanzania imeainisha maeneo mbalimbali ya kuangazia katika uwekezaji kwenye Bahari ya Hindi, yakiwemo nishati, uvuvi, usafirishaji, utalii pamoja na michezo.
“Tunataka kuangazia fursa zote zilizopo kwenye Bahari yetu ya Hindi: fursa kwenye maeneo ya nishati, fursa kwenye maeneo ya uvuvi, fursa kwenye maeneo ya usafirishaji, fursa kwenye maeneo ya utalii pamoja na michezo,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa mwenyekiti wa jukwaa la Mkataba wa Nairobi kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, ambapo imekuwa ikisimamia mambo yaliyomo ndani ya mkataba huo, yakiwemo uhifadhi wa rasilimali za bahari na matumizi endelevu ya rasilimali hizo.
Alisema pia wamekuwa wakisimamia namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa bahari pamoja na kuendelea kutumia fursa za uchumi wa buluu zinazopatikana baharini.
Alisema moja ya maazimio yanayotarajiwa kutoka katika Mkutano wa 12 wa Mkataba wa Nairobi ni kupata mwendelezo wa uhifadhi wa rasilimali za bahari ili ziwe na matumizi endelevu.
“Kwa maana tutatoka na kitu kinaitwa Dar es Salaam Declaration (Azimio la Dar es Salaam), ambalo kimsingi hasa linalenga usalama wa uhifadhi wa bahari yetu na rasilimali zake,” alisema.
Alisema jukwaa hilo la biashara limewaleta pamoja wadau mbalimbali kwa lengo la kupata maazimio ya pamoja kuhusu namna ya kuendelea kutumia fursa za uchumi wa buluu katika Bahari ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Mkutano wa 12 wa Mkataba wa Nairobi unaendelea jijini Dar es Salaam ukiwa na vikao na majukwaa mbalimbali vinavyojadili masuala ya uhifadhi katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.



