Zungu akagua athari za korongo mpwapwa

Apr, 19 2020

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu mwishoni mwa wiki amefanya ziara ya kikazi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kukagua athari zilizosababishwa na korongo kubwa kando ya Mto Shaban Robert.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo aliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya haraka kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ili kunusuru wananchi kuzingirwa na maji yanayojaa katika mto huo.

Waziri Zungu alisema pamoja na hayo Serikali kupitia Ofisi yake imeichukua changamoto hiyo na kuahidi kukaa na wataalamu wa mazingira kuanza utekelezaji wake. "Athari hii sio ndogo ni kubwa na inahitaji uangalifu mkubwa katika kuitatua kwani kila siku maji yanaongezeka katika mto huu, pia sisi kama Serikali tumetenga fedha za kukabiliana na maafa kama kupitia mifuko ya kitaifa na ya kimataifa hivyo tutazama tuone nini tunafanya," alisema.

Aidha Waziri Zungu aliwataka wananchi kuendelea kushiriki katika suala zima la uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti na kuitunza ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.

Settings