​Zungu abaini ukosefu wa cheti cha mazingira machimbo ya kaolin Kisarawe

Jun, 22 2020

Zungu abaini ukosefu wa cheti cha mazingira machimbo ya kaolin Kisarawe

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amefanya ziara katika eneo la machimbo ya madini ya kaolin yanayomilikiwa na kampuni ya Rakkadlin Co. Ltd wilayani Kisarawe lenye changamoto za kimazingira ikiwemo kutokuwa na cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira.

Mhe. Zungu ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Jokate Mwegelo, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Anorld Mapinduzi, wanasheria kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC pamoja na viongozi mbalimbali katika wilaya ya Kisarawe ambapo amejionea shughuli za uchimbaji wa madini hayo yanayotumika kutengenezea malighafi za marumaru.

“Tumepitia matamko ya mwekezaji na ya wataalamu wetu na tumeona tatizo lipo. Mwekezaji alipewa masharti toka mwaka 2018 arekebishe lakini mpaka leo bado hajayarekebisha. Biashara inaendelea na malalamiko ya wananchi bado yapo. Kwahiyo Mhe. DC tutakupa matokeo yafindings zetu kwa mwanasheria wa NEMC na wa Ofisi ya Rais ni hatua zipi ambazo tutazichukua.” Amesema Mhe. Zungu

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mhe. Jokate Mwegelo amesema wahusika wa eneo hilo wanaonekana kutokujali kabisa juu ya utaratibu uliopo na kuwataka kuheshimu sheria.

“Hapa inavyoonekana kuna uholela, vitu havijakaa sawa.Na mheshimiwa Waziri nadhani na wewe umejionea. Sio kwamba hatuhitaji wawekezaji, Sio kwamba Kisarawe haina mali lakini muhimu sheria na taratibu zifuatwe. Hayo yote yakifuatwa hata wananchi wangekuwa wanafurahia mradi.” Amesema Mhe. Mwegelo

Nae Meneja wa NEMC kanda ya Mashariki Bw. Anold Mapinduzi amesema kuwa mwekezaji anayehusika na mradi huo anatakiwa kufuata utaratibu wa kimazingira ili kuepusha madhara zaidi.

“Anavyoelekezwa kuzingatia yale matakwa ya kimazingira kuendana na sheria na kanuni ni kwa faida yake.Wananchi wakiathirika hataweza kulipa hayo maisha ya wananchi. Wananchi wakitoka na kuja kumharibia kutokana na kushindwa kuridhika kutokana na vitendo anavyowafanyia itakuwa ni hasara kwake. Kwahiyo ni vizuri anavyopewa maelekezo akayatekeleza kwa wakati.” Amesema Mapinduzi

Mmiliki wa Machimbo hayo bwana Adam Iremu amesema kuwa anasubiri muafaka wa mgogoro huo atakapoitwa naMhe. Waziri kama alivyoeleza.

“Kikubwa ni wakishaniita nitakwenda na mimi nitoe ushahidi wangu na vielelezo vyangu na ndio nitafahamu maamuzi watakayo yatoa.” Amesema Iremu

Machimbo ya madini ya Kaolini katika eneo hilo la Kisarawe yanamilikiwa na kampuni ya Rakkadlin Co. Ltd na wamiliki hao kwa muda mrefu wamekuwa wazito kutekeleza maagizo wanayopewa na mamlaka mbalimbali za mazingira ikiwemo NEMC pamoja na mamlaka za serikali ya Wilaya ya Kisarawe.

Settings