Zungu aahidi wananchi Hanang Serikali kunusuru Ziwa Bassotu

Apr, 04 2020

Serikali imeahidi kuchukua hatua za haraka kunusuru Ziwa Bassotu wilayani Hananag mkoani Manyara kutokana na kujaa na kufurika maji ambayo yamezingira makazi ya wanachi wa eneo hilo.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu alipotembelea eneo hilo kujionea athari hizo zilizotokana na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.

Katika ziara hiyo akiwa ameambatana na wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) aliahidia kuwa Serikali itatumia wataalamu hao kufanya utafiti ili kupata suluhisho la kudumu.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo walioathirika na mafuriko aliwaahidi kuliweka suala hilo katika miradi ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kupata fedha zitakazosaidia kulitatua.

“Tumetazama tatizo hili hapa panahitaji utaalamu mkubwa tutachukua hatua kwani tunaona eneo lote la ziwa limeingiwa udongo na kufanya maji yafurike na tunaweza kudhani maji ni mengi kumbe wakati wa kiangazi tutakuwa na shida ya maji kwa hiyo kuweni na Imani na Serikali yenu tutalifanyia kazi,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Joseph Mkirikiti alisema athari zilizotokana na mafuriko hayo ni uharibifu wa miundombinu ikiwemo nyumba za wakazi wa eneo hilo kuzingirwa na maji.

Aidha, Mkirikiti aliongeza kuwa sema kwa takriban wiki tatu sasa kumekatika mawasiliano kati ya eneo hilo na Haydom ambapo barabara iliyo kando mwa ziwa hilo haipitiki kutokana na kujaa maji.

Mkuu huyo wa wilaya aliomba mamlaka zinazohusika ziweze kuchukua hatua kwa wakati ili kunusuru wananchi hao wasipate madhara Zaidi kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji.

Hata hivyo itakumbukwa hivi karibu iliagizwa barabara ya Haydom – Katesh isitumike ili kuepusha madhara kwa watumiaji kutokana na kufurika kwa maji hayo.

Akizungumza kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Hifadhi ya Mazingira wa NEMC, Lilian Lukambuzi alisema tatizo hilo limetokea kutokana na shughuli mbalimbali za binadamu.

Lukambuzi alisema kuwa panapaswa kufanyika utafiti kama ambavyo Waziri alielekeza pamoja na kuweka mipango ya muda mfupi na mrefu kwa ajili ya kunusuru ziwa hilo.

Alisema kuwa moja ya hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa ni pamoja na kuzuia shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo hayo ambazo ndizo chanzo cha tatizo hilo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Hanang Mhe. Dkt. Mary Nagu alionesha hofu yake ya ziwa hilo kuweza kujaa udongo kutokana na mito inayotoka maeneo mbalimbali na hivyo kukosekana kwa maji.

Alimshuruku waziri huyo kwa kufika na wataalamu kutoka NEMC chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na kujionea madhara mbalimbali yanayotokana na kufurika kwa mto huo hivyo kuwa tayari kuyafanyia kazi.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Ziwa Basotu ni chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi wa Wilaya ya Hanang katika Mkoa wa Manyara.

Settings