Waziri Zungu: Wakiukaji Sheria ya Mazingira kukiona

Feb, 05 2020

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amewaonya wachimbaji wadogo wa dhahabu wanaokiuka sheria ya mazingira kwa kushindwa kudhibiti kemikali ya zebaki na kutiririka ovyo.

Zungu alitoa onyo hilo jana wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Butiama mkoani Mara alipotembelea eneo la wachimbaji wadogo Sirori Simba na Buhemba.

Katika ziara hiyo ambayo pia aliitumia kusikiliza kero za wachimbaji hao wadogo na kuangalia uzingatiaji wa sheria ya mazingira yam waka 2004, waziri huyo alibainisha kuwa kemikali ya zebaki ina madhara kwa afya na mazingira.

Alisema kwa sasa bado haujapatikana mbadala wa kemikali hiyo lakini ni wajibu wa wachimbaji hao kuitumia kwa uangalifu ili kuhakikisha haisambai ovyo na kusababisha uchafuzi wa hasa kwenye vyanzo vya maji, mifugo na kilimo.

“Elimu iendelee kutolewa kuhusu madhara ya kutotumia zebaki kwa uangalifu na hali kama hii itawafanya wananchi wetu waugue na wakiugua Serikali inaingia gharama ya kuwatibu maradhi yanayotokana na udhaifu wa kushindwa kusimamia mazingira vizuri,” alisema Zungu.

Aidha katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababisha changamoto ya mabadiliko ya tabianchia aliwaonya kuacha kukata miti wanayotumia kuimarisha kuta za mashimo na badala yake watumie njia nyingine mbadala.

Waziri huyo aliwataka wachimbaji wadogo kupanda miti ma wanavyofanya wa ajili ya kuitumia katika migodi na kusema kuwa huo ni uharibifu wa mazingira hivyo akawataka wapande miti kwa wingi ili kuhifadhi mazingira.

“Ndugu zangu wachimbaji wadogo Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ameanzisha masoko ya madini na nyie munge mkono kwa kuhifadhi mazingira, mpande miti kwa wingi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine Waziri Zungu ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia ofisi zake za kanda kuacha mara moja utaratibu wa kuwatoza wachimbaji wadogo bila kuwapa elimu.

Akiwasilisha malalamiko hayo mbele ya waziri, Mwenyekiti wa Wachimbaji wadogo mkoa wa Mara, John Liyamera aliiomba Serikali kupitia maafisa mazingira wawe wanawatembelea wachimbaji kuwapa elimu.

Alidai wachimbaji hao wako tayari kulipa tozo ili kuongeza mapato ya Serikali lakini kinachowakwamisha ni kuwa hawapati elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Settings