Waziri Zungu atoa mwito kwa wawekezaji kufuata sheria

Mar, 01 2020

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema wawekezaji wanapaswa kutimza matakwa ya sheria ya uhifadhi wa mazingira sambamba na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Zungu ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza katika viwanda vya kutengeneza mifuko mbadala aina ya non woven vya Jin Yuan Investment, CMG Pyramid na Hoteli ya Malaika katika Wilaya ya Ilemela.

Alikagua uzalishaji wa mifuko hiyo na kujionea shughuli za uhifadhi wa mazingira alisema kuwa nia ya Serikali ni kujenga urafiki na wawekezaji katika sekta ya viwanda na ndio maana imeweka masharti yasiyo magumu ili waweze kuendelea kuwekeza na hivyo maendeleo yapatikane.

“Viwanda vinachangia ajira na pato la ndani kwa kulipa kodi lakini vinapaswa kuzingatia matakwa ya sheria na tunasisitiza mifuko mbadala yenye ubora ambayo ni rafiki wa mazingira na pia inaongeza pato la nchi kwani wanalipa kodi.

Settings