Waziri Zungu aonya wazalishaji mifuko mbadala isiyokidhi viwango

Feb, 08 2020

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa wazalishaji na wasambazaji wa mifuko isiyokidhi viwango ili kudhibiti uchafuzi utokanao na mifuko hiyo.

Zungu alitoa kauli hiyo Itigi Wilayani Manyoni mkoani Singida leo baada ya kushuhudia zoezi la uteketezaji wa zaidi ya tani 11.53 za mifuko mbadala aina ya non-woven iliyokamatwa katika mikoa ya Tabora, Singida na Dodoma.

Katika zoezi hilo lililofanyika kwa kutumia kichomeo taka cha kisasa cha Hospitali ya Mt. Gaspar iliyopo wilayani humo aliwataka wananchi kutonunua mifuko isiyokidhidhi viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kufanya hivyo watengenezaji hawatapata soko na hivyo itaisha.

“Mifuko hii ni michafu na inaharibu mazingira, Serikali imeshatoa agizo na sheria imetungwa lakini mifuko hii inarudi hapa wafanyabiashara wana kiburi wanadharau mamlaka na sisi tutachukua hatua stahiki, lakini tutaendelea kutoa elimiu kwa wananchi” alisisitiza Zungu.

Alitoa rai kwa wazalishaji, wasambazaji na wananchi kwa ujumla kuwa ni kosa kisheria kutumia mifuko aina ya non-woven isiyokidhi viwango vya ubora na hatutasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote au kiwanda kitakachozalisha mifuko mbadala isiyokidhi viwango vya ubora.

Aliongeza kwa kuhamasisha jamii itumie mifuko yenye viwango Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwani watengenezaji wa mifuko hawalipi kodi na inachafua mazingira na pia kutasaidia kuinua viwanda vyetu.

Aidha waziri huyo katika ziara hiyo aliyotumia pia kutembelea masoko na maduka na kutoa elimu kuhusu matumizi ya mifuko mbadala alilielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuendelea na ukaguzi wa mifuko isiyokidhi viwango na hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Awali katika taarifa yake Meneja wa Kanda ya Kati wa NEMC Novatus Mushi alisema katika operesheni hiyo, Baraza likishirikiana na wataalamu kutoka TBS, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa husika (REME), Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya husika, Jeshi la Polisi na idara nyingine za serikali walifanya ukaguzi katika maeneo ya masoko, maduka ya bidhaa za vyakula, na stoo za kusambaza bidhaa mbalimbali.

Alisema katika zoezi hilo, jumla ya tani 3.03 za mifuko iliyopigwa marufuku ilikamatwa. Aidha, kufuatia operesheni za awali zilizofanywa na NEMC Juni hadi Mushi alifafanua kuwa Desemba, 2019 kiasi cha tani 8.5 za mifuko iliyopigwa marufuku na ile isiyokidhi viwango ilikamatwa hivyo, kufanya jumla ya kiasi cha mifuko iliyokamatwa kufikia tani 11.53.

Zoezi hilo lilishuhudiwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Solomoni, Kamati ya Ulinzia na Usalama ya Wilaya hiyo na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

Settings