Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Waziri Ummy azitaka Wizara zenye hoja za Muungano kuzipatia ufumbuzi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Wizara ambazo zina hoja 11 za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kukaa mara moja ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.

Waziri Ummy ameyasema hayo hii leo katika kikao cha pamoja baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.

Amesema tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha tunaimarisha Muungano wetu na kuhakikisha una kuwa imara kwasababu Muungano wetu ndio umoja wetu, usalama wetu na amani yetu.

“Hatutamvumilia mtu yoyote anayeleta chokochoko na kutaka kuvuruga umoja na mshikamano wa watanzania” Ummy alisisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Khalid Mohammed amesema Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanya kazi kubwa katika kuondoa changamoto kumi ndani ya kipindi cha miaka mitano.

“Kupitia vikao vya Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ndani ya kipindi cha miaka mitano jumla ya changamoto 21 ziliwasilishwa na kati ya hizo changamoto 10 zimepatiwa ufumbuzi, ni imani yangu kuwa hata zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi kwa kuwa viongozi wetu wana dhamira ya dhati” amesisitiza Dkt. Khalid.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar imeanza matayarisho ya ujenzi katika kiwanja chenye ukubwa wa ekari 33 katika eneo la Mahoma Makulu ili kurahisha kazi ya uratibu.

“Hakuna sababu ya sisi kubaki Dar es Salaam, tutahakikisha tunahamia Dodoma mapema iwezekanavyo ili kufanya kazi kwa karibu”

Waziri Ummy amemuhakikishia Waziri Khalid kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano.