Waziri Mkuu akemea utiririshaji wa maji machafu

Jun, 05 2022

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amekemea tabia ya utiririshaji wa maji machafu na majitaka kutoka viwandani na kwenye migodi kwani inachangia kuhatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira.

Alitoa onyo hilo Juni 5, 2022 wakati akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Mhe. Majaliwa alisema hivi karibuni tumeshuhudia kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai, maeneo mengi ya vyanzo vya maji yameathirika kutokana na ukame wa mara kwa mara, uchafuzi wa mazingira unaotokana na majitaka na kemikali kutoka na shughuli za viwandani.

Aidha, Waziri Mkuu aliongeza kwa kusema kuwa uchafuzi huu umeendelea kuongezeka kwa kasi nchini na kuathari maji, hewa na ardhi.

Vilevile, alikemea tabia ya uchomaji miti, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu.

“Kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira, ninaagiza Wizara na taasisi husika, pamoja na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano katika kukomesha uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu kote nchini. Ninawasihi wananchi tutoe ushirikiano wa kutosha kuhakikisha tunarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo yetu, hususan maeneo ambayo miti ya asili iko kwenye tishio la kutoweka. Tuwe walinzi wazuri wa mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho,” alisisitiza.

Akizungumza na washiriki wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Fedha na Mipango inapaswa ihakikishe Mpango Kabambe wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira unakuwa sehemu ya vipaumbele vya bajeti vya kila mwaka kwa kipindi chote cha utekelezaji wake wa miaka 10.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo alisema Ofisi yake imezindua Kampeni ya Soma na Mti ambapo kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti mmoja.

“Tumezindua Kampeni ya Soma na Mti ambapo wanafunzi milioni 14.5 kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu wameshiriki kwa kupanda mti mmoja mmoja.

Waziri Mkuu alizindua Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamamizi wa Mazingira na kutoa tuzo kwa Mabalozi wa Mazingira na viongozi wakuu watano akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yalichagizwa na Wiki ya Mazingira iliyoenda sambamba na shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira jijini Dodoma ambapo kwa mwaka huu kaulimbiu ilikuwa “Tanzania ni Moja Tu, Tunza Mazingira”.Waziri Mkuu alizindua Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamamizi wa Mazingira na kutoa tuzo kwa Mabalozi wa Mazingira na viongozi wakuu watano akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Settings