Waziri Jafo: Mliovamia Bonde la Ihefu muondoke haraka

Nov, 15 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaagiza wananchi waliovamia Bonde la Ihefu kuondoka mara moja kwani kitendo hicho kinasababisha uharibifu wa mazingira.

Amesema hayo Novemba 15, 2022 wakati akizungumza katika kikao cha mawaziri nane wa kisekta, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wataalamu kilichofanyika katika Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyoko mkoani Iringa.

Dkt. Jafo alisema kuwa hali hali ya kutotiririka kwa maji kwa miezi kadhaa katika mto huo imesababishwa na kitendo cha wananchi kuvamia vyanzo hivyo vya maji.

Alitaja sababu za kukauka kwa mto huo ni uingizaji wa mifugo ndani ya Bonde la Usangu na kwenye ardhi oevu ya Ihefu, uchepushaji wa maji kutoka kwenye mito inayoingiza maji Bonde la Usangu unaofanywa na baadhi ya wakulima wasiofuata sheria na taratibu.

Pia, alitaja sababu zingine kuwa ni pamoja na vitendo vya ukataji holela na uchomaji wa misitu unaosababisha ukame na uharibifu wa mazingira.

Hivyo alisema ili kunusuru hali hiyo Mamlaka za Bonde za Maji zinapaswa kusimamia Sheria iliyopitishwa na Bunge 2022 inayoelekeza wale wote wanaochepusha maji kinyume cha sheria kuchukuliwa hatua.

Alielekeza pia mamlaka hizo na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kubaini wale wote waliovamia vyanzo vya maji waondoke mara moja.

Settings